Ndugai awafunda CUF bungeni


Spika wa Bunge, Job Ndungai
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amevitaka vyama vya Upinzani kuacha kuwavua au kuwasimamisha uanachama wabunge wao kwa maelezo kuwa jambo hilo ni gharama kwa Taifa, chama husika na ukatili kwa wananchi waliowachagua.

Ingawa hakutaja chama alichokilenga, hivi karibuni Baraza Kuu la Uongozi la CUF lililokutana Zanzibar, lilimsimamisha uanachama Mbunge wake wa Kaliua, Magdalena Sakaya kutokana na kilichoelezwa ni kuvunja Katiba kwa kutohudhuria kikao bila taarifa.

Mbunge mwingine aliyekumbwa na rungu hilo ni Maftaha Nashuma (Mtwara Mjini), aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama wengine wanane.

Akizungumza baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu bungeni jana, Ndugai alisema: “Vyama vya Upinzani vimekuwa na utaratibu wa kufukuza wabunge wao, ningependa vyama hivi vijifunze kutoka CCM ambacho sijawahi kusikia kikifukuza mbunge miaka ya karibuni.”

Ndugai alisema kitendo cha CCM kutofukuza wabunge wake hakimaanishi kuwa wawakilishi hao wa wananchi ni malaika, kwamba wapo vichwa ngumu.

“Hawafukuzi hovyo maana kupata mbunge wa kuchaguliwa ni shughuli pevu. Mbunge si lazima achaguliwe na wanachama wa chama husika, pia anaweza kuchaguliwa na wananchi wengi lakini ninyi mnakaa wachache na kumfukuza,” alisema.

Alisema kitendo cha mbunge kufukuzwa kinasababisha gharama kubwa kumpata mwingine, huku akiomba radhi kwa kauli yake hiyo baada ya wabunge wa Upinzani kuonekana kukerwayo.

“Nimeomba radhi mapema msinishambulie nitoe tu mawazo yangu, ni vizuri tukipata mbunge tuvumiliane naye, haya mambo madogo madogo si tumalize huko ndani (ya chama) na katika hili muiige CCM maana inafanya mazuri,” alisisitiza.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo