Mdee, Tibaijuka, Lyimo ‘wateka’ Bunge


Halima Mdee
BUNGE limepitisha Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa ya Mwaka 2016, huku wabunge watatu wakiibana Serikali kutaka baadhi ya vifungu vibadilishwe.

Msimamo wa wabunge hao uliibua mvutano kati yao na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Abdallah Possi.

Muswada huo wenye vifungu 24, ulifanyiwa marekebisho katika vifungu zaidi ya 15 yakiwamo marekebisho ya Serikali huku Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akitengua kanuni za chombo hicho cha kutunga sharia, kilipokaa kama kamati juzi jioni, ili kikao kiendelee na hadi Muswada huo utakapopitishwa kifungu kwa kifungu.

Wabunge waliokuwa wakizungumza kwa kupokezana kusimama bungeni mithili ya watu waliokuwa wamepanga jambo hilo tangu awali, ni Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), Halima Mdee (Kawe) na Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema).

Kabla ya kupitishwa kwa Muswada huo, Dk Mwakyembe alijibu hoja za wabunge walizotoa wakati wa mjadala na kubainisha kuwa haukusudii kudhibiti vyombo vya habari, bali kuviongeza wigo wa upatikanaji wa taarifa, huku akiwashukia wabunge wa upinzani na kuwapiga kijembe kwa uamuzi wa Chadema kumpokea Edward Lowassa na kumpitisha kuwa mgombea urais katika uchaguzi uliopita.

Licha ya juhudi za wabunge hao kutaka mabadiliko ya vifungu hivyo, baadhi ya mapendekezo yao yalipanguliwa na Masaju na mawaziri hao na kuwezesha vifungu hivyo kupita kama vilivyo.

Katika kifungu cha pili, Profesa Tibaijuka alitaka kibadilishwe ili kulinda watu kutumia mamlaka vibaya, kusumbua taasisi binafsi kudai taarifa kwa madai ya kuwa na maslahi ya umma.

Licha ya Mbunge huyo kutaka hoja hiyo ijadiliwe na wabunge wengine, Mwenyekiti Chenge ambaye alikuwa akiingilia kati pale malumbano kati ya wabunge na mawaziri hao yalipokuwa makali, alipangua hoja hiyo.

Tibaijuka aliibuka tena wakati wa kupitisha kifungu cha tatu, lakini aliondoa hoja yake kwa kuwa ya kifungu cha pili ilikataliwa, huku Lyimo akiibuka katika kifungu cha tatu akitaka utolewe ufafanuzi wa neno mtu wa tatu jambo ambalo lilipingwa na Masaju na Possi.

Mdee pia alitaka marekebisho katika kifungu hicho kwa maelezo kuwa lazima sheria imtaje mtu wa tatu ni nani, jambo ambalo Dk Mwakyembe alilijibu na kufafanua kuwa suala hilo likiibua ukakasi, litabadilishwa.

Vifungu vingine vilivyopingwa na wabunge hao wakitaka marekebisho ni kifungu cha nne, sita, tisa, 12,13, 15,18, 20, 22 na 23.

Kwa upande wa Serikali ilifanya marekebisho yakiwamo ya kuondoa makosa katika Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 ambayo yaliingizwa kwenye Muswada huo.

Awali ilipendekezwa adhabu ya kifungo jela kati ya miaka 15 hadi 20 kwa mtu atakayebainika kutenda makosa kuhusu na kukiuka maslahi ya Taifa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo