Makonda: Oktoba mosi kupanda miti



Suleiman Msuya

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ametangaza siku ya Oktoba mosi mwaka huu itakuwa siku ya kupanga miti katika mkoa wake ambapo vyombo vya usalama vitashiriki.

Makonda aliyasema hayo jana katika mkutano wa 14 wa wahandisi nchini ikiwa ni siku moja baada ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza kuahirisha maandamano na mikutano nchi nzima Oktoba mosi iwapo hakutakuwa na muafaka kati ya viongozi wa dini na Rais John Magufuli kuhusu madai yao ya kutaka kufanya mikutano.

Chadema ilikuwa imetangaza kufanya maandamano na mikutano kupitia kivuli cha Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), Septemba mosi ila waliahirisha kwa madai kuwa wameombwa na viongozi wa dini ili wamuone rais.

Alisema baada ya jana kufanya usafi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ikiwa ni maadhimisho ya miaka 52 ya jeshi hilo aliona ni vema wakaanzisha kampeni ya upandaji miti katika mkoa huo.

“Ndugu zangu wahandisi mimi nimejipanga kushirikiana nanyi na katika kuonesha hilo Oktoba mosi itakuwa siku ya kupanda miti Dar es Salaam ambayo itabeba kauli mbiu ya ‘mti wangu’,” alisema.

Aidha, alitumia mkutano huo wa wahandisi kuwaomba kufanya mijadala ya kitaaluma na kuwa vyombo vya usalama vitawapatia ulinzi na kuwa hataruhusu mikutano na malumbano yasiyo na tija.

Mkuu huyo wa mkoa alisema wananchi wa Dar es Salaam wanapaswa kufanya kazi na kuachana na tabia ya kuzurura kwani hawatawavumilia.

Baada ya kauli hiyo baadhi ya washiriki wa mkutano huo walisikika wakinung’unika kwa kudai kuwa upo uwezekano wa Serikali kupata mtikisiko wa Ukuta jambo ambalo linasababisha kupanga matukio yanayogongana na mipango ya Chadema.

“Naona sasa kila kukicha jamaa wanateseka hali ambayo inawalazimu kila linalopabgwa na Chadema nao wanapanga kufanya jambo sidhani kuwa huu ndio uongozi unaotakiwa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo