Hofu bado yatawala Vikindu


IGP Ernest Mangu
TAHARUKI imeendelea kuwakumba wakazi wa kijiji cha Vikindu Mashariki kulikotokea mauaji ya Kamanda wa Kikosi cha Kudhibiti Ujambazi na majibizano ya risasi baina ya polisi na majambazi, hadi leo siku ya 14 tangu tukio hilo.

Usiku wa Agosti 26 polisi waliokuwa wakifuatilia majambazi waliovunja na kuiba katika benki ya CRDB Mbande, Dar es Salaam, walijikuta katika mapambano na majambazi hao waliowakuta eneo la Vikindu wilayani Mkuranga.

Uchunguzi wa JAMBOLEO umebaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara sasa wanafunga maduka yao mapema, huku wakazi wake wakilazimika kurudi majumbani mapema zaidi ikilinganishwa na kabla ya tukio hilo.

Wakati staili ya maisha ikionekana kubadilika, nyumba iliyoshambuliwa na polisi, imeonekana kutelekezwa, baada ya vifaa vyake kuendelea kuwa nje ya nyumba hiyo tangu siku hiyo, huku taa zake zikiwa zinawaka muda wote.

Maduka kufungwa

Mwenyekiti wa Kijiji cha Vikindu Mashariki, Mohammed Maundu alisema hali katika kijiji hicho ni tofauti ikilinganishwa na awali kutokana na baadhi ya maduka kufungwa mapema. Alisema mbali na maduka kufungwa mapema, ya karibu na nyumba kulikofanyika mapambano hayo, bado yameendelea kufungwa kutokana na wamiliki kuchukuliwa na Polisi kwa mahojiano zaidi.

Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya maduka yakiwa na makufuli, huku baadhi ya wahusika wakishikiliwa na Jeshi hilo.

Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya wafanyabiashara wanafanya biashara zao kwa uoga na waendesha pikipiki wamekuwa wakisitisha huduma hiyo giza linapoingia kutokana na uoga.

Hatukuwajua watu hao

Mwenyekiti huyo alisema hakuwafahamu watu wanaodhani kuwa ni majambazi, ingawa taarifa alizopata baadaye zilieleza kuwa walikuwa hapo siku nyingi.

“Kuna watu wanasema watu hao walikuwa hapo karibu miaka mitatu sasa na wengine wanasema wana miezi sita tu. Mimi sina hakika kwani sikuwafahamu kabla,” alisema Mwenyekiti huyo ambaye alimtupia lawama mjumbe wa eneo hilo kwa alichosema ni kutompa taarifa mapema.

Mgogoro wa viongozi

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa hana ushirikiano mzuri na viongozi wenzake wa Serikali na hili lilitokana na mseto unaounda Serikali hiyo ya kijiji. Alisema katika kipindi cha mfumo wa chama kimoja viongozi walielewana, lakini sasa mfumo wa vyama vingi katika eneo hilo umesababisha changamoto.

Alipata taarifa za ujambazi? Mwenyekiti huyo alieleza kuwa alipigiwa simu na kuitwa eneo la tukio ambako alifika saa tatu asu-buhi. “Kiutaratibu suala hilo ndivyo linavyofanyika lakini jambo lililonishangaza ni baadhi ya wananchi kuwa na fikra tofauti na kuhisi kwamba Mwenyekiti huyo anahusika kwenye suala hilo,” alisema.

Mwenyekiti alitoa mwito kwa viongozi wa eneo hilo, hususan wajumbe wa nyumba 10 kushirikiana katika masuala mbalimbali, akibainisha kuwa jukumu la kulinda amani ya eneo linaanzia kwao.

“Hatuwezi kulinda wenye silaha za moto, lakini vibaka inawezekana na ni jambo la kitaifa, hivyo inabidi viongozi wa eneo hili na kwingine kushirikiana nasi badala ya kumwachia majukumu mtu mmoja,” alisema.

Gazeti hili lilishuhudia vitu vikiwa vimetawanywa na kutelekezwa nje ya nyumba hiyo. Ndani ya vyumba kulikuwa na vitu kama vyerehani, nguo za watoto, mabegi, majiko, matundu ya vyoo yalikuwa wazi, paa la nyumba liliharibiwa lote huku ukimya ukitawala katika aneo hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo