Celina Mathew
Zitto Kabwe |
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo)
amesema suala la Serikali kukaa na wawekezaji si jawabu la tatizo lililotokea bali
kinachotakiwa ni Katiba Mpya yenye kumilikisha utajiri wa nchi kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Zitto imekuja siku moja baada ya Rais John Magufuli
kukutana na Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambaye ni mmiliki
mkubwa wa Kampuni ya Acacia Mining Limited, Profesa John Thornton na
kukubaliana kampuni hiyo kufanya mazungumzo na Serikali yake.
Pia Profesa Thornton alisema kampuni yake itakuwa tayari kulipa
fedha ambazo Tanzania imepoteza kutokana na uendeshaji wa shughuli zake nchini
ikiwa italazimika baada ya majadiliano.
Hatua ya kampuni hiyo kufanya mazungumzo na Rais Magufuli
inatokana na taarifa ya Kamati ya pili
ya wachumi na wanasheria iliyopewa jukumu la kuchunguza mikataba ya madini na
kiwango kilichopo kwenye makanikia yaliyosafirishwa nje na kwenye kontena 277
zilizozuiwa bandarini Dar es Salaam.
Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alipokea taarifa ya Kamati
hiyo ambayo ilieleza kuwa Acacia haijasajiliwa na haipo kisheria nchini, jambo
ambalo liliibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii na maeneo mengine hususan kwa
wanasiasa.
Lakini akizungumza Dar es Salaam jana, Zitto ambaye ni
Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo alisema chama chake kilihadharisha jambo hilo
katika kongamano lake la Rasilimali Madini lililofanyika Juni 3 Dar es Salaam.
“Tulihadharisha hili Juni 3 kwamba mwisho wa siku
Serikali itakaa mezani, hivyo tuombe sana hoja za Serikali ziwe na ushahidi wa
kutosha, vinginevyo tutaendelea kulia kuibiwa daima,” alisema.
Aliongeza kuwa jawabu la changamoto zilizojitokeza si mazungumzo
na wawekezaji, bali ni Katiba mpya yenye kumilikisha utajiri wa nchi kwa
wananchi wa Tanzania milele, ambao ndio rasilimali yao.
Juni 3 ACT-Wazalengo ilifanya kongamano la Rasilimali
Madini la kujadili nchi inavyonufaika na
sekta ya madini ambalo liliibuka na maazimio 10, likiwamo la kutaka mjadala
mpana kulinda aina zote za madini nchini.
Watoa mada
katika kongamano hilo lililenga kujadili kwa kina sekta hiyo baada ya hivi
karibuni Rais John Magufuli kuunda Kamati ya Kuchunguza Mchanga wa Madini
unaosafirishwa nje na kutoa ripoti iliyoshitua Taifa.
Kongamano hilo
lilihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa
Vitendo (LEAT), Dk Rugemeleza Nshala, Mwenyekiti wa Taasisi ya ONGEA, Dennis
Mwendwa na Nico Kajungu wa Numet.
Kamati
iliyochunguza mchanga wa madini chini ya uenyekiti wa Profesa Abdulkarim Mruma,
ilibaini kuwa kontena 277 zilizozuiwa katika bandari ya Dar es Salaam zina tani
7.8 za dhahabu yenye thamani ya kati ya Sh bilioni 676 na Sh trilioni 1.147.
Kiwango hicho
kilikuwa tofauti na ambacho Kamati hiyo ilielezwa na Wakala wa Ukaguzi wa
Madini (TMAA) kwamba kontena hizo zilikuwa na tani 1.1 za dhahabu.
ACT-Wazalendo
ilieleza kuwa mbali na kutaka uchunguzi ufanyike kwa madini yote, kongamano hilo
lilibaini kuwa takwimu za Kamati zina walakini.
“Takwimu hizi zikikubaliwa kama zilivyo, zitaifanya
Tanzania kuwa mzalishaji namba moja wa dhahabu Afrika. Hatuhitaji kupika
takwimu au kuongopa, ili kushinda vita vya rasilimali.
“Kunapaswa kuwa na timu huru ya kupitia takwimu
zilizotolewa na Kamati ya Profesa Mruma ili kuthibitisha uhalali wake. Kuwa na
takwimu sahihi ni muhimu sana kwenye kupata majawabu,” lilieleza azimio la
pili.
Azimio lingine ni kwamba katika mapambano ya
kulinda rasilimali madini, ni lazima yafanyike mabadiliko ya sheria ya madini
na Katiba, ili kufanya madini na maliasili zingine kuwa mali ya wananchi
milele.
“Serikali ibadilishe mfumo wa kuchimba madini kwa
kuhamia kwenye mfumo wa kugawana mapato ili kuondokana na mfumo wa sasa ambao
kimsingi una njia nyingi za kukwepa kodi kwa mbinu halali kabisa,” kilieleza
chama hicho katika azimio lake la nne.
Pia kilitaka sauti za wafanyakazi katika migodi
ziheshimiwe, haki zao zilindwe na washirikishwe kikamilifu kwenye uamuzi kuhusu
sekta ya madini.
“Mikataba ya madini izingatie kuwa kuna uharibifu
wa mazingira kwenye uchimbaji madini. Mikataba iwe na vifungu imara vya kulinda
mazingira.
“Watu wote walioshiriki kuingia mikataba ya madini
na kufanya uamuzi unaolitia Taifa hasara wawajibishwe na kuchukuliwa hatua bila
kujali vyeo vyao au lini makosa yalifanyika.”
Katika azimio la nane, kongamano hilo lilipendekeza
kufanyika kwa usanifu wa madini ya tanzanite likisema: “Sisi ndio wazalishaji
pekee wa tanzanite. Hivyo tuna ukiritimba unaotuwezesha kushawishi kampuni za
vito vya tanzanite kujenga viwanda Tanzania.”
Pia lilitaka mikataba yote ya madini ipitiwe upya,
kama ikihitajika kurekebishwa ifanyike hivyo ili kulinda maslahi ya umma,
kwamba iwapo mikataba husika itabainika kuwa ya hovyo ivunjwe kama ilivyotokea
katika nchi za Bolivia, Venezuela, Iran na Botswana.
“Mjadala wa rasilimali madini usiachwe mikononi mwa
Serikali ya CCM ambayo ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo sasa,” lilieleza azimio
la 10 la kongamano hilo.
“Wananchi wote kupitia asasi za kiraia, vyama vya
siasa na umma kwa ujumla washiriki kuhakikisha mjadala juu ya rasilimali madini
unafikishwa mwisho kwa maslahi ya umma.”
0 comments:
Post a Comment