Mwandishi Wetu
Waziri Joyce Ndalichako |
CHUO cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC)
kimeanzisha masomo ya Shahada ya Kwanza ya Uhazili na Utunzaji Kumbukumbu,
Taarifa na Nyaraka.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa
Chuo hicho, Dk Henry Mambo alitoa mwito kwa watumishi wa umma na Watanzania
wenye sifa, kuchangamkia nafasi hizo za masomo kwa manufaa yao binafsi na
Taifa.
Dk Mambo alisema masomo hayo yataanza Septemba
katika matawi ya Dar es Salaam na Tabora na mengine yatafuata.
Alisema mwombaji anatakiwa kuwa na elimu
ya kidato cha sita na ufaulu wa masomo mawili au Diploma katika fani husika
yenye ufaulu au GPA ya alama 3.
Mkuu huyo alifafanua, kwamba masomo hayo
ya ngazi ya Shahada yameanzishwa ili kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanaongeza
elimu kwenye fani hiyo na kupanua soko la ajira.
“Kutokana na mabadiliko ya teknolojia na
mifumo ya utendaji kazi ni vema watumishi wa umma na Watanzania wenye sifa, wakapata
mafunzo ya kuwawezesha kukabiliana na changamoto katika soko la ajira,” alisema.
Alibainisha, kwamba mafunzo hayo yatawezesha
wahitimu kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha zaidi na hivyo kuchangia uendelezaji
na ukuaji wa taaluma ya utunzaji kumbukumbu, taarifa na nyaraka.
Katibu Mkuu wa Chama cha Makatibu Mahsusi
Tanzania (TAPSEA), Festo Melkiory alisema kuanzishwa kwa kozi hizo ni fursa kwa
Watanzania hususan makatibu mahsusi na watunza kumbukumbu.
Alisema matumaini yake ni kuona kozi
hizo zinaongeza weledi na ujuzi miongoni mwa watumishi wa umma na Watanzania.
“Hiki kilikuwa ni kilio chetu cha siku
nyingi, sasa kimesikilizwa, ni matumaini yangu kuwa makatibu mahsusi wengi
wataichangamkia fursa hii,” alisema.
0 comments:
Post a Comment