Celina Mathew
Zitto Kabwe |
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe
amesema uamuzi wa Serikali kulifunga gazeti la Mawio kwa miaka miwili unapaswa
kulaaniwa na kila mwanademokrasia na kwamba ni hofu.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alionya
vyombo vya habari vinavyotaka marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete
kuhusishwa na sakata la mchanga wa madini.
Wakati Rais akitoa katazo hilo, juzi gazeti
hilo kwenye ukurasa wake wa mbele lilichapisha picha za marais hao wastaafu likiwahusisha
na sakata la mchanga wa madini.
Pia katika ukurasa wa 12 wa gazeti hilo,
yalichapishwa makala ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ikionesha kuwatuhumu
viongozi hao kuhusu sakata hilo huku wakiwa hawakutajwa kwenye taarifa za uchunguzi
wa kamati za Rais.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Zitto alidai
kuwa uhusika wa marais hao wastaafu kwenye mikataba ya madini ulisemwa na Rais
Magufuli na si Mawio.
“Hakuna mkataba ulioingiwa bila Baraza
la Mawaziri kuidhinisha. Kitendo cha Kamati ya Rais kutuhumu mawaziri wa zamani
mbele ya Rais Magufuli na yeye kusema hatapona mtu, ilikuwa ni dhahiri kuwa
Rais anawachimba watangulizi wake,” alisema.
Alisema kwa kuwa wao ni watu
waliofundishwa lugha ya uongozi, waliamua mapema kuwa Rais Magufuli alikuwa anatuhumu
wenzake na kwamba gazeti hilo lilitafsiri maelezo yake.
“Kwa sisi tuliofundishwa lugha ya uongozi
tuling'amua mapema kuwa Rais Magufuli alikuwa anatuhumu wenzake. Hivyo Mawio ilitafsiri
tu maelezo ya Rais,”alisema na kuongeza:
“Kitendo cha Rais kuonya kuwa marais
wastaafu waachwe ilikuwa ni kujisemesha tu na kufungia Mawio ni hofu ya Rais
baada ya kuwasema watangulizi wake. Kila wakati Rais analia kuhujumiwa na
kutaka kuombewa, adui wa Magufuli ni Magufuli mwenyewe.”
Aliitaka Serikali kulifungulia gazeti hilo
mara moja bila masharti, kwani kulifunga ni kuwanyima Watanzania mawazo mbadala
kuhusu mambo ya hovyo yanayoendelea nchini.
Serikali kupitia Idara ay Habari,
MAELEZO juzi ilitangaza kjulifunga Mawio kuchaowa kwa muizei 24 kuanzia juzi,
kutokana na Mamlaka aliyonayo Waziri mwenye dhamana ya habari kwa mujibu wa
kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016.
0 comments:
Post a Comment