Is-Haka Omar, Zanzibar
UMOJA wa
Wanawake wa Tanzania (UWT) umewataka wanawake kuchangamkia fursa za
uongozi kwnye uchaguzi unaondelea sasa ndani ya CCM na jumuiya zake.
Mwito
huo ulitolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo Zanzibar, Tunu Juma Kondo
katika mwendelezo wa ziara ya UWT kuzungumza na viongozi wapya wa
ngazi za matawi kwenye jimbo la Kijini, wilaya ya Kaskazini A, Unguja.
Aliwaambia wanawake
kuwa uchaguzi unaoendelea kwenye taasisi hiyo ndiyo fursa mojawapo ya
wanawake kupata uongozi ili kufikia malengo ya uwakilishi wa viongozi wenye idadi
sawa na wanaume ndani ya chama hicho.
Alifafanua
kuwa wanawake wanatakiwa kuondokana na dhana ya kuendelea kuongozwa katika
kila nafasi ndani ya CCM bali wajiongeze kuwania uongozi ili kuleta maendeleo
endelevu ndani ya chama na jumuiya zake.
Pia
alisisitiza viongozi hao kuwa, pamoja na majukumu ya kiuongozi waliyonayo ni
lazima wahamasishe kwa wingi wanawake kuwania uongozi ili kupata viongozi
makini na wenye uwezo wa kwenda na kasi za kiutendaji za chama hicho.
"Wanawake
wenzangu tutumie fursa ya uchaguzi wa chama kuwania uongozi, tusisubiri uteuzi tusimame
kupambana na kuhakikisha nasi tunakuwa na nyadhifa kama walivyo wanaume, kwani
tunaweza bila kuwezeshwa,’’ alisema Tunu.
Akizungumza
kwenye ziara hiyo, Katibu Msaidizi wa Idara ya Organaizesheni ya UWT Zanzibar, Mgeni
Ottow alisema CCM itadumu madarakani endapo viongozi wanaopatikana kupitia
uchaguzi wa chama hicho watakuwa na uzalendo wa kweli katika kulinda maslahi ya
taasisi
Mgeni
aliwasihi wanawake wa Umoja huo kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu
na wenye uwezo wa kubuni fursa za maendeleo zitakazonufaisha wanawake wenzao na
chama kwa ujumla.
“Wanawake
ndilo tegemeo la chama chetu na jumuiya kwa ujumla hivyo lazima tuwe wa kwanza
kujitokeza kwa kila tukio kuhusu uimarishaji wa chama chetu hasa michakato ya
uchaguzi na tukiwa wengi katika nafasi za uongozi, ndipo tutakapopata nguvu za
pamoja kutetea haki zetu na kupinga kisheria udhalilishaji wanawake,” alisema
Mgeni.
Mwenyekiti
wa UWT wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Miza Ali Kombo alisema uchaguzi wa ngazi ya
wodi unaendelea vizuri, kwani wagombea tayari wamejaza fomu na kinachosubiriwa
sasa ni upigaji wa kura ili kupata viongozi watakaoongoza ngazi hiyo kwa miaka
mitano.
Katibu
wa UWT wa Tawi la Muange, Waja Mnadhani Ali alisema maratajio yake baada ya
kupata nafasi hiyo, ni kufanya kazi za jumuiya na chama kwa umakini na uadilifu,
ili kuwawakilisha vema wanawake waliomwamini na kumpa ridhaa.
0 comments:
Post a Comment