Grace Gurisha
Kitilya na wenzake |
UPANDE wa mashitaka, katika kesi inayomkabili aliyekuwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili, umeieleza Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa wamepokea awamu ya kwanza ya vielelezo vya
upelelezi kutoka Uingereza.
Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali, Christopher
Msigwa mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wa Mahakama hiyo wakati kesi
hiyo ilipotajwa.
Msigwa alidai kuwa bado wanasubiri awamu ya pili ya
vielelezo na kwamba wanatarajia vitafika wakati wowote kuanzia sasa.
Baada ya kudai hivyo, Wakili wa utetezi, Mwanahamisi Adam
aliomba upande wa mashitaka ueleze muda mwafaka utakaotumika vielelezo hivyo
kufika nchini.
Hakimu Mkeha alisema huo muda uliotajwa na upande wa mashitaka
uwe ndani ya simu 14 na ikishindikana Juni 30 waeleze vitafika ndani ya siku
ngapi.
Mbali ya Kitilya, wengine ni mshindi wa Mashindano ya
Urembo mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon.
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa kutenda
makosa kati ya Machi 2013 na Septemba mwaka juzi, wakati wa mchakato wa mkopo
wa dola milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka benki ya Standard ya Uingereza.
Washitakiwa hao wanadaiwa kula njama na kujipatia fedha kwa
njia za udanganyifu na kutakatisha fedha.
Sinare katika kesi hiyo, anadaiwa kuwa
Agosti 2, 2012 alighushi kwenye makao makuu ya benki ya Stanbic, Kinondoni
kwa nia ya kudanganya ambapo aliandaa
nyaraka za mapendekezo akijaribu kuonesha kuwa Standard ikishirikiana na Stanbic
wangetoa mkopo wa dola milioni 550 kwa Tanzania
kwa ajili ya ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo, wakati
akijua kuwa si kweli.
Inadaiwa kuwa Agosti 2, 2012, Sinare alitoa nyaraka za
uongo za mapendekezo kuonesha kuwa Standard ikishirikiana na Stanbic wangetoa mkopo wa dola milioni 550 na kuziwasilisha kwenye ofisi za Hazina wakati akijua kuwa si kweli.
Pia anadaiwa kuwa Septemba 20, 2012 katika makao makuu ya Stanbic, Kinondoni, alighushi barua ya mapendekezo
ikionesha kuwa Standard ikishirikiana na Stanbic wangetoa mkopo wa dola milioni 550 kwa Tanzania kama ada ya uwezeshaji wa asilimia 2.4 ya
kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.
0 comments:
Post a Comment