Octavian Kimario, Dodoma
Ramo Makani |
SEIKALI imesema wazo la kuwarudisha nchini Dinosaria kutoka
Ujerumani halina tija kutokana na ugumu wa kiteknolojia na gharama
ikilinganishwa na faida za hatua hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Ramo Makani akijibu swali la Mbunge wa Mchinga, Hamidu
Bobali (CUF) aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu faida ambayo wananchi wa
Lindi na Tanzania kwa jumla wanaipata kutokana na mabaki hayo.
Makani alisema Tanzania itaendelea kusisitiza kupata
manufaa kutokana na Dinosaria wake walioko Berlin, Ujerumani.
“Kutokana na majadiliano ya kina yaliyohusisha wataalamu
wabobezi katika masuala ya malikale kutoka pande zote mbili, ilikubalika kuwa
Serikali ya Ujerumani itaendesha shughuli za utafiti zaidi Tendaguru na maeneo
jirani.
“Nia ni kuwezesha uchimbaji mabaki ya Dinosaria wengine
yanayoaminika kuwepo maeneo hayo pamoja na kuanzisha Kituo cha Makumbusho ili
shughuli za utalii zifanyike eneo hilo na kuvutia watalii wa ndani na nje ya
nchi,” alisisitiza Makani.
Kuhusu Serikali kupunjwa mapato yatokanayo na viingilio kwenye
Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin, Makani alisema jambo hilo halina ukweli.
Alisema ni ngumu kufahamu kiasi ambacho hupatikana kutokana
na kiingilio kuwaona mijusi wa Tanzania, kwa kuwa Makumbusho hayo yana kumbi
nyingi zenye masalia kutoka nchi kadhaa za Afrika na gharama za kuendesha
Makumbusho hayo hutolewa na Serikali ya Ujerumani.
Alieleza kuwa Serikali hiyo itafadhili uimarishaji wa
idara inayohusika na malikale katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwezesha upatikanaji
wataalamu wa kutosha wa fani hiyo ili kuendeleza utalii wa malikale nchini.
Mabaki ya mijusi hayo wakubwa (Dinosaria) yalichimbwa kwenye
kilima cha Tendaguru mkoani Lindi kati ya mwaka 1909 na 1913 na kupelekwa kwenye
Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin.
0 comments:
Post a Comment