SICHUAN, China
Zhang Liyong |
BABA aliyekata tamaa mkazi wa China
vijijini amechimba kaburi kwa ajili ya binti yake anayeugua ili “kumwandaa kwa
kifo chake”.
Zhang Liyong, mkulima wa jimbo la
Sichuan, ametumia akiba yake yote kumtibu mwanawe huyo, ambaye alizaliwa akiwa
na tatizo kubwa la damu.
Baba huyo alisema amekuwa akimpeleka
binti yake huyo mwenye miaka miwili kaburini hapo kucheza na kupumzika kila
siku ili “alizoee eneo hilo ambalo anatarajiwa kuzikwa.”
Video iliyotumwa na kampuni ya Pear
Video imeonesha tukio hilo linalogusa nyoyo za watu, lililotokea jijini
Neijiang, Kusini Magharibi mwa China.
Kwenye video hiyo, baba anaonekana
amelala ndani ya kaburi hilo huku amempakata binti yake huyo, Zhang Xinlei.
Xinlei aligundulika na ugonjwa
ujulikanao kama thalassemia, ugonjwa wa kurithi unaohusu damu, akiwa na umri wa
miezi miwili.
Zhang na familia yake walitumia zaidi ya
yuan 100,000 (pauni 11,490) kumtibu Xinlei, lakini wakashindwa kuendelea kumudu
gharama hizo za matibabu.
“Tulikopa fedha kutoka kwa watu wengi,
lakini kwa sasa hawako tayari tena kutukopesha,” Zhang alisema.
Wawili hao walifikiria kuzaa mtoto
mwingine ili wapate damu ya kiunga mwana ili itumike kumwokoa Xinlei. Hata
hivyo, waligundua kuwa hatua hiyo isingewezekana baada ya mke wa Zhang kupata
ujauzito.
“Tumebanwa. Hatuna chaguo lingine,” Deng
Min ambaye ni mama wa binti huyo alisema. Waliamua kukata tamaa ya tiba na
kujielekeza kwenye maandalizi ya kifo cha Xinlei.
“Hili ndilo wazo pekee nililobaki nalo –
kumleta kucheza hapa. Hapa ndipo mahali atakapopumzika milele kwa amani.
Ninachoweza kufanya ni kuja naye hapa kila siku,” baba huyo, Zhang alisema.
Anatumaini kwamba Xinlei atalizoea kaburi
hilo na hivyo hatakuwa na hofu siku ikiwadia.
Thalassemia ni ugonjwa wa damu wa
kurithi. Kwa mujibu wa NHS, watu wenye hali hiyo hutengeneza kidogo au
hawatengenezi kabisa himoglobini, ambayo hutumiwa na seli nyekundu za damu
kusafirisha hewa ya oksijeni mwilini.
Watu wenye tatizo hilo huhitaji tiba ya
maisha yote kwa kuwekwa damu nyingine kila mara au tiba ya Chelation.
0 comments:
Post a Comment