Grace Gurisha
MFANYABIASHARA Casto Ngogo (35), amepandishwa kizimbani kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya
kukutwa na vifaa vya Serikali ambavyo ni suruali 5,000 za sare ya Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Ngogo ambaye ni mkazi wa Tabata, Segerea, Dar es Salaam
alifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa kusomewa mashitaka
yanayomkabili.
Wakili wa Serikali, Hamisi Saidi alidai kuwa Juni 15,
maeneo ya Bandari Kavu ya Galco, Chang'ombe, Temeke, Dar es Salaam, Ngogo
alikutwa na suruali hizo 5,000 za JWTZ kwenye kontena namba PCIU 82851 (5) zikiwa
na thamani ya Sh milioni 59 mali ya Serikali bila kibali.
Baada ya kusomewa mashitaka, Ngogo alikana kuhusika na
tuhuma hizo, ambapo upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo
haujakamilika na hauna pingamizi na dhamana.
Hakimu Nongwa alisema ili mshitakiwa awe nje kwa dhamana
anatakiwa awe na fedha taslimu Sh milioni 30 au hati ya mali isiyohamishika
yenye thamani hiyo na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh milioni 10
kila mmoja.
Ngogo alitimiza masharti hayo na kuachwa huru na kesi
hiyo iliahirishwa hadi Julai 17 itakapotajwa.
0 comments:
Post a Comment