Is-Haka Omar, Zanzibar
Zanzibar |
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dk Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’, amewasihi
wananchi wa shehia ya Ndagoni mkoani Kusini Pemba
kulinda miundombinu ya majisafi na salama isiharibiwe na baadhi ya watu wenye
tabia ya kuhujumu miundombimu hiyo kwa makusudi.
Nasaha hizo alizitoa jana wakati
akikagua miundombinu ya maji iliyotengenezwa na Mamlaka ya Maji Pemba
baada ya kuharibiwa na watu wasiojulikana ambayo kwa sasa imerudiswa
hali ya kawaida na wananchi wameanza kupata huduma hiyo.
Dk Mabodi alisema nishati ya maji ni muhimu kwa
maisha ya kila siku kwa wananchi wote, hivyo ni lazima miundombinu yake
ithaminiwe na kuwekewa ulinzi wa kudumu kwani ikikosekana
wanaoteseka ni wananchi wasio na hatia hasa wagonjwa na wazee wasiojiweza.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwambia wananchi hao kuwa siasa
za chuki na migogoro zimepitwa na wakati, hivyo wabadilike na
kuanza kuishi kwa misingi ya umoja na ushirikiano kwa lengo la kuharakisha
maendeleo ya kisiwa hicho.
Aidha, alieleza kwamba dhamira ya CCM ni kufanya siasa
zenye ushindani wa kutatua kero za wananchi, ili kupata huduma bora za
kijamii zitakazonufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Aidha, Dk Mabodi alitoa pole kwa
wananchi wa kisiwa cha Pemba waliopata mafuriko ya mvua kubwa za masika na
kusababisha uharibifu wa mali na vifo, na kwamba CCM inashirikiana na Serikali
kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.
“Mwezi uliopita nilikuja hapa na kutoa agizo kwa ZAWA washughulikie
tatizo hili na wananchi wapate maji safi na salama, nakupongezeni kwa
kutekeleza agizo langu kwa wakati na naendelea kupita maeneo mengine
kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema Dk Mabodi.
0 comments:
Post a Comment