Mwandishi Wetu
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amevionya vyombo vya habari vinavyowataja marais
wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete vikiwahusisha na taarifa za kamati
mbili za uchunguzi wa makinikia zilizokabidhiwa kwake.
Dk Magufuli alitoa onyo hilo jana, siku tatu baada ya kupokea
ripoti ya Kamati ya pili aliyounda ikiongozwa na Profesa Nehemiah Osoro ambayo
ilichunguza maeneo ya kisheria na kiuchumi kuhusu mikataba ya madini na mchanga
wa madini.
Hata hivyo, baada ya kupokea ripoti hiyo, wadau wa masuala ya
mikataba ya madini wakiwamo wanasheria na wanasiasa, wamekuwa wakihusisha
mikataba hiyo mibovu ya madini na viongozi wastaafu wa awamu ya tatu na nne,
Mkapa na Kikwete maelezo ambayo yamekuwa yakiripotiwa na vyombo vya habari.
Hata hivyo, Rais Magufuli amezuia wastaafu hao kutajwa akisema: “Nimesoma
ripoti zote mbili hakuna mahali ambapo Mzee Mkapa na Mzee Kikwete wametajwa,
vyombo vya habari viache kuwachafua hawa wazee, wamefanya kazi kubwa ya
kulitumikia Taifa letu, viwaache wapumzike.”
Kauli hiyo ya Rais Magufuli imo katika taarifa yake iliyotumwa kwa
vyombo vya habari ambayo baadaye ilikaziwa na Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.
Akikazia onyo hilo la Rais, Dk Mwakyembe alisema: “Ikumbukwe
kwamba taarifa iliyotolewa na Kamati haikuwataja, wala kuwatuhumu marais hao
wastaafu na Serikali ya Awamu ya Tano…, inawaheshimu na kutambua mchango wao
adhimu katika kujenga ustawi wa nchi yetu.”
Aliongeza: “Naviasa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii
kuacha mara moja mwelekeo huo hasi, ambao una kila dalili ya kututoa kwenye
mstari na kupotosha kampeni tuliyonayo ya kujikomboa kiuchumi.”
0 comments:
Post a Comment