Suleiman Msuya
Jiji la Dar es Salaam |
MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya
Mwita amewaasa wananchi wa jiji hilo kudumisha amani, mshikamano, upendo na
ushirikiano ili kuweza kufanikisha mipango mbalimbali waliojiwekea.
Mwita aliyasema hayo mwishoni mwa wiki
wakati akizungumza na wananchi waliowaalika katika hafla ya futari iliyofanyika
viwanja vya Ofisi ya Meya vilivyopo kwenye Ukumbi wa Karimjee.
Alisema amani inayoonekana kuwepo
kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan inapaswa kuwa endelevu ili kuchochea
ujenzi wa jiji hilo.
Meya alisema iwapo jamii ya Dar es
Salaam itazingatia amani, mshikamano, upendo na ushirikiano ni dhahiri kuwa
mipango mbalimbali waliyojiwekea itafanikiwa.
“Tunahitaji maendeleo katika sekta
mbalimbali njia sahihi ya kufikia huko tunapaswa kuwa na amani, umoja,
mshikamona, ushirikiano na upendo hivyo naamini kupitia Ramadhan na futari hii
tutakuwa na mwanzo mzuri,” alisema.
Aidha, alitumia futari hiyo kuwataka
viongozi mbalimbali wa Jiji la Dar es Salaam kujikita katika kutoa huduma za
kijamii ili kuwatatulia wananchi changamoto zinazowakabili.
Meya Mwita alisema iwapo kila kiongozi
atasimamia majukumu yake ipasavyo itakuwa rahisi kwa Serikali kufikia malengo
ya kuboresha huduma za kijamii.
Aliwataka wananchi kuitumia ofisi yake
ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili na wasisubiri mpaka hali iwe mbaya
ndio wamtafute.
“Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba
wananchi wa Dar es Salaam kutumia ofisi ya jiji ipasavyo kwani ipo kwa ajili
yenu mimi nipo tayari kuwasikiliza,” alisema.
0 comments:
Post a Comment