Dalila Sharif
BARAZA la Vijana Chadema (BAVICHA) limekemea
baadhi ya viongozi wanaotumia madaraka vibaya kwa kuwakamata viongozi wa chama
hicho kwa kutumia nguvu za madaraka yao.
Pia Baraza limesema liko tayari
kumfungulia kesi Mkuu wa Wilaya ya Ubongo, Kisare Makori kwa kukiuka na
kuingilia muhimili wa mamlaka husika katika kumwamuru Meya wa Ubongo, Boniface Jacob
akamatwe bila sababu za msingi.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Baraza
hilo, Potrabas Katambi akisema ukamataji viongozi wa chama hicho umeendelea
kukua kwa kasi, huku baadhi ya viongozi wa chama tawala wakitumia madaraka yao
kunyanyasa viongozi wa vyama pinzani.
Alisema hali hiyo inakiuka taratibu za
mamlaka husika kufanya kazi zake na kuingilia viongozi wenye majukumu yao
mengine kwa kutumia sheria vibaya.
“DC wa Ubungo ametumia mamlaka vibaya kuamrisha
kumkamata Meya wa Jimbo hilo kwa kudhaniwa kuwa anafanya mkutano jambo ambalo
si kweli,” alisema Katambi.
Alisema vitendo vya wakuu wa wilaya na
mikoa kutumia madaraka yao kukamata watu ni uonevu wa hali ya juu, hali ambayo
haiwezi kufumbiwa macho na chama chake.
Aidha, amewataka viongozi kutoingilia
madaraka ya chombo husika na kulitaka Jeshi la Polisi kusimamia wenye haki na
si kupewa amri na baadhi ya viongozi ili kukomoa watu.
“Mchezo huu tunaomba usitishwe mara moja,
kwa sababu viongozi wa namna hii wanatafuta kiki za kupata umaarufu na si kutumikia
jamii katika kutatua changamoto zao,” alisema Katambi.
Alisema upinzani si vita, bali ni kuibua
changamoto za hamasa kwa chama tawala katika kufanya kazi kwa bidii, hivyo
kutumiwa vibaya vyama vya upinzani ni upotoshaji wa amani.
Hata hivyo, tukio la kukamatwa kwa Meya
huyo lilitokea Jumatatu saa sita mchana makao makuu ya wilaya hiyo yaliyo
Kibamba baada ya kuzuia msafara huo, ulioshirikisha viongozi wa Chadema akiwamo
Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye na viongozi wengine wa Ubungo na Kanda ya
Pwani.
Pia alimwomba Rais John Magufuli,
kusimamia vema suala la mchanga wa madini (makinikia) na Akaunti ya Escrow kwa
kuwataka viongozi waliohusika na hayo kuchukuliwa hatua mara moja.
0 comments:
Post a Comment