Grace Gurisha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemfutia
kesi ya kuishi nchini bila kibali Mwanasheria Mkuu wa Shirika la Viwango
Tanzania (TBS), Baptister Bitaho (54).
Hata hivyo, baada ya mshitakiwa huyo kuachwa huru jana alikamatwa
tena na yupo Idara ya Uhamiaji akihojiwa.
Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo, baada ya Mwendesha
Mashitaka wa Uhamiaji, Method Kagoma kuiomba Mahakama imfutie kesi chini ya
kifungu cha 98(a) cha sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).
Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa alikubaliana na maombi
hayo na kuifuta kesi hiyo, ambayo mshitakiwa alikuwa anakabiliwa na mashitaka
matatu.
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Uhamiaji, Novatus Mlay alidai
kuwa Mei 19 maeneo ya Kinondoni katika ofisi ya Uhamiaji, Bitaho akiwa raia wa
Burundi, alikutwa nchini bila kibali cha kumwezesha kuishi nchini.
Alidaiwa kuwa Bitaho siku hiyo alikutwa akifanya kazi
kama Mwanasheria Mkuu wa TBS bila kibali kinachomruhusu kufanya kazi nchini.
Alidai kuwa Julai 6, 2011 katika ofisi ya Uhamiaji ya Mkoa
wa Dar es Salaam wilayani Ilala, mshitakiwa huyo akiwa raia wa Burundi, alitoa
taarifa za uongo kuhusu maelezo yake binafsi, wakati akijaza fomu ya kuomba
hati ya kusafiria namba CT (5)(Ai).
Wakili Mlay aliongeza kuwa kitendo hicho cha kutoa
taarifa za uongo kilimwezesha Bitaho kupata hati ya kusafiria ya Tanzania yenye
namba AB 474856 huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria za nchi.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, alikana na upande wa
mashitaka kudai kuwa upelelezi bado haujakamilika na alikuwa nje kwa dhamana baada
ya kukamilisha masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika,
ambao kila mmoja alisaini dhamana ya Sh milioni 20.
0 comments:
Post a Comment