Abdallah Amiri, Igunga
Dk Dalaly Kafumu |
BAADHI ya wananchi wa hapa wamemtaka Mbunge wao Dk Dalaly
Kafumu ajiuzulu ubunge kwa walichodai ni kushindwa kutumia madaraka yake vizuri
wakati akiwa Kamishna wa Madini.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wilayani
hapa, baadhi ya wananchi hao, Oscar Thomas, Godfrey Batoba, Pius Roben na Regina
Jackson, walisema ni vema mbunge wao akajiuzulu kwa kuwa miongoni mwa wanaotuhumiwa
kuiingizia hasara nchi kwa kuingia mikataba mibovu ya madini na kujinufaisha.
Thomas alibainisha kuwa kazi anayofanya Rais John Magufuli
ya kufuatilia rasilimali za wananchi inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania
mwenye uchungu na nchi yake huku wakimwomba kutoonea huruma wahusika walioisababishia
nchi hasara.
Mwenyekiti wa Wazee wa Wilaya, Kassim Ally akizungumza
kwa niaba ya wazee wenzake, alisema walimwomba Rais Magufuli kutokatishwa tamaa
na baadhi ya viongozi wasio waaminifu kwani wako nyuma yake wakimpa
ushirikiano.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya, Costa Ollomi na wakem,
Mwanamvua Killo walisema kazi anayofanya Rais Magufuli imeleta heshima ndani ya
chama na Serikali na kuwataka wananchi kuendelea kuwa watulivu wakati
waliohusika wakihojiwa na vyombo husika.
Kuhusu Mbunge kujiuzulu alisema Ollomi alisema hawezi
kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari Rais alishatoa maelekezo ya kuchukuliwa
hatua kwa waliotajwa na Kamati.
Gazeti hili lilimtafuta Dk Kafumu kupitia simu yake ya
kiganjani ili kuzungumzia matakwa hayo lakini hakupokea
simu licha ya kupigiwa zaidi ya mara nne.
0 comments:
Post a Comment