WASHINGTON, DC, Marekani
Donald Trump |
KARIBU wabunge 200 wa Democrats wamesema
watafungua mashitaka dhidi ya Rais Donald Trump wakidai kuwa kuendelea kwake
kujihusisha na biashara zake kunakiuka Katiba ya nchi.
Mashitaka hayo yatamtuhumu Trump kwa
kukiuka Kifungu cha Maslahi cha Katiba ya Marekani, ambacho kinakataza maofisa
wa Serikali kupokea zawadi au wadhifa kutoka serikali za kigeni bila
kuidhinishwa na Bunge, kwa mujibu wa wabunge wanaoongoza azma hiyo.
Kesi hiyo itakuwa na walalamikaji wengi
kuliko kesi yoyote iliyopata kufunguliwa dhidi ya Rais katika historia ya Taifa
hili, kwa mujibu wa Mbunge wa Michigan, John Conyers, ambaye yuko kwenye Kamati
ya Bunge ya Sheria.
“Hatufanyi hivi kujifurahisha au
kupendelea, lakini ni kwa kuwa Rais Trump ametufanya tushindwe kufanya
vinginevyo,” alisema.
Shirika la Trump linajumuisha zaidi ya
kampuni 500 za kibiashara zilizo kwenye takriban mataifa 20 duniani, na
zinahusisha hoteli, viwanja vya gofu na nyumba za makazi, nyingi zikifanya
biashara na serikali za kigeni.
Serikali hizo zimelipia matukio
mbalimbali kwenye hoteli za Trump na ada za matengenezo ya vyumba katika
majengo ya Trump.
Ingawa Shirika la Trump limeahidi kutoa
faida zitokazo kwenye Serikali hizo katika biashara ya hoteli kwa ajili ya
Hazina ya Marekani, waraka wa sera za kampuni uliotolewa mwezi jana, unaonesha
kuwa mali za Trump hazitathibitisha kama wateja binafsi ni wawakilishi wa
serikali za kigeni kibiashara.
Seneta Richard Blumenthal wa
Connecticut, alisema mashitaka hayo ni ya lazima ili kumlazimisha Trump aweke
hadharani ni kwa kiasi gani kampuni zake zinaendesha biashara na serikali za
kigeni na kuruhusu Bunge kutekeleza majukumu yake ya kikatiba ya kutoa au
kutotoa ruhusa chini ya Kifungu cha Maslahi.
“Hatuwezi kuruhusu tusichokijua,”
alisema. “Anaingilia wajibu wetu wa kikatiba.”
Trump na wanasheria wake wamesema kifungu
hicho hakihusiki na miamala ya soko la haki na kwamba alishachukua hatua za
kujiondoa kwenye biashara zake.
Hata hivyo, wakfu ambamo Trump amewekeza
mali zake unaendeshwa na wanawe wa kiume. Trump ni mnufaika pekee wa wakfu huo
na anaweza kuchukua fedha muda wowote atakao.
Anatarajiwa kupokea taarifa za fedha za
biashara yake wakati wote akiwa madarakani. Ni rais pekee katika historia ambaye
hajawasilisha nakala ya marejesho yake ya kodi.
Wabunge hao walisema watawasilisha
malalamiko yao Jumatano asubuhi kwenye Mahakama ya Wilaya ya Marekani ya
Washington DC. Kesi hiyo inataka uamuzi wa Mahakama unaosema Trump anahusika na
Kifungu cha Maslahi na amri ya kumtaka Trump asipokee zawadi.
Wabunge hao wanawakilishwa na Kituo cha
Uwajibikaji Kikatiba, kilichoko DC ambacho ni cha kisheria “kilichopo kwa ajili
ya kukidhi utekelezaji wa Katiba.”
Kutokana na kutofautiana kwa kanuni za
kimaadili za Bunge na Baraza la Seneti, maseneta watatenganisha gharama za
uwakilishi wa kisheria. Kituo hicho cha Uwajibikaji Kikatiba kitatoa huduma za
kisheria kwa wabunge hao.
0 comments:
Post a Comment