*JPM akutana Ikulu na Mwenyekiti wa Barrick
*Timu yake na
ya Tanzania kukaa kujadiliana
Suleiman
Msuya
Rais John Magufuli |
RAIS John Magufuli amesema kampuni Barrick Gold Corporation
imekubali kulipa fedha zitakazobainika kuwa inadaiwa kutokana na uchimbaji
madini wanaofanya nchini, baada ya mazungumzo.
Alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya
kuzungumza na Mwenyekiti wa Barrick yenye asilimia 64 ya hisa za Acacia,
Profesa John Thornton aliyefuatana na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles wakimshirikisha
Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi.
Profesa Thornton alikuja nchini siku tatu baada ya Kamati Maalumu
ya Kuchunguza Masuala ya Kisheria na Kiuchumi kuhusu mchanga wenye madini
unaosafirishwa nje ya nchi kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Magufuli ikionesha
Taifa kupata hasara.
Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe wanane wakiongozwa na Profesa
Nehemiah Osoro, wengine wakiwa ni Profesa Longinus Rutasitara, Dk Oswald
Mashindano, Gabriel Malata, Casmir Kyuki, Butamo Kasuka, Usaje Asubisye na
Andrew Massawe.
Kwa mujibu wa ripoti yake, Kamati hiyo ilibainisha kuwa mikataba
ya madini tangu mwaka 1998 ndiyo ililisababishia Taifa upotevu wa takriban Sh
trilioni 108.46 ambazo zingetumika kwenye bajeti ya miaka mitatu kwa kuakisi
bajeti ya mwaka 2017/18 huku baadhi ya mawaziri na wanasheria wakitajwa kushiriki
kuikosesha Serikali mapato hayo.
Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Magufuli alisema mazungumzo
yao yalikwenda vizuri na Mwenyekiti huyo wa Barrick aliridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa
na Serikali.
Rais Magufuli alisema Barrick italeta timu itakayofanya kazi na
timu ya Tanzania kupitia ripoti zote ili kufikia mwafaka.
“Wameridhika na juhudi tulizofanya kama Serikali na kuwa wamesikia
kilichofanywa, lakini ataleta timu yake ili kupitia mapendelezo na timu yetu,”
alisema na kuongeza:
“Profesa Thornton amekubali chochote kitakachokubalika watalipa,
uzuri alikuwepo Profesa Kabudi, mwanasheria. Nikafurahi nikasema hawa ni wanaume,
lakini pia wakasema ni bahati mbaya, wanatubu kwa yalitokea.”
Rais Magufuli alisema Serikali inakaribisha mazungumzo baina ya
pande hizo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na Barrick,
ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha
shughuli zake nchini kwa maslahi ya pande zote mbili.
Alisema pamoja na kukubali kulipa fedha inazodaiwa, Profesa Thornton
alikubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu nchini.
Profesa Thornton alisema walikuwa na majadiliano mazuri yatakayowafikisha
mahali ambapo kila mmoja atafaidika na uwekezaji huo.
“Nimekuja hapa kuzungumza kuhusu yanayowasibu Acacia, ili tuweze
kufikia mwafaka na nimemwahidi Rais kuwa tutakuwa na mazungumzo mazuri ambapo
kila mtu atafaidika, hivyo timu zetu zitakutana mapema iwezekanavyo,” alisema.
Kamati ya Pili ya Rais Magufuli ilitoa mapendekezo 21 kwa Serikali
ikiwamo kutaka mawaziri waliohusika na mikataba hiyo kuanzia mwaka 1998,
wanasheria wakuu na manaibu wao na watumishi wa wizara wahojiwe ili ukweli
ujulikane.
0 comments:
Post a Comment