CHADEMA yabebea bango Serikali na makinikia


Dalila Sharif

Dk Vincent Mashinji
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka Serikali iombe radhi Watanzania na iwe tayari kuwajibika, kwa kuwaongoza vibaya kiasi cha kuporwa rasilimali zao kwa miaka 20 ya nyuma.

Kauli hiyo imekuja wakati chama hicho kikitoa msimamo kuhusu ripoti ya Kamati ya pili ya kuchunguza kontena zenye mchanga wa madini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vincent Mashinji, alisema CCM inatakiwa kijitafakari kama bado ina uhalali wa kisiasa kuendelea kuwa madarakani.

Alisema kila aliyehusika kurasimisha wizi na uporaji huo, anatakiwa kuwajibika kwa mujibu wa sheria hata kama ni mkubwa kwa kiwango gani.

“Rais hatafaulu vita hivi kama Serikali yake itaendelea na utamaduni wa kutubagua au kutosikiliza sauti za upande wa pili, ni vema akajua kuwa hata ilanai ya chama chake ukurasa wa 26 na 28, hazungumzii kabisa hoja za mikataba na sheria za madini kuhitaji kurekebishwa upya,” alisema Mashinji.

Alisema wameshangazwa na kitendo cha Rais kuimarisha mawazo ya uadui dhidi ya watu wenye maoni tofauti, wakati ametoka kuliomba Taifa liwe pamoja naye katika vita vya kutetea rasilimali.

“Rais kama anataka uwazi katika vita hivi, ni vema arudishe Bunge lioneshwe mbashara, ili Watanzania waone na kujua wabunge wa vyama vyao, ambao ni mawakala wa uporaji rasilimali za Taifa letu, ili wawahukumu katika uchaguzi ujao,” alisema Mashinji.

Alisema dhamira ya kweli ya Rais katika mapambano hayo, ikiwa ni pamoja na kuweka wazi mikataba iliyoingiwa kwa siri kati ya Serikali ya CCM na wawekezaji, isiishie kwenye mikataba ya madini peke yake.

Alitaka mikataba yote iwekwe hadharani, ikiwemo ya sekta ya ujenzi, uuzwaji nyumba za Serikali na mashirika ya umma, ili kunusuru rasilimali ya Taifa.

Alisema ni vema Watanzania wakaelezwa kuhusu sheria na mikataba iliyoingiwa na Serikali na wawekezaji hao kwa kuwa ni haki yao, hata kama kweli makinikia hayo yana thamani kubwa kiasi hicho cha matrilioni yaliyotajwa.

Mashinji alisema Chadema inamtaka Rais atoe hadharani ripoti zote za makinikia, kwani kuna maswali mengi yasiyo na majibu juu ya jinsi sampuli zilivyochukuliwa.

Maswali mengine kwa mujibu wa Mashinji ni utaratibu uliotumika katika maabara ya kupimia sampuli husika na njia iliyotumika kufikia hitimisho la kiwango cha dhahabu na madini yaliyo kwenye mchanga huo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo