Mwandishi Wetu
UTAFITI uliofanywa na taasisi ya Twaweza
umebaini kuwa asilimia 71 ya Watanzania wanaukubali utendaji kazi wa Rais John
Magufuli ingawa kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 96 ikilinganishwa na
ulipofanyika Juni mwaka jana.
Utafiti huo unatokana na takwimu za
Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa
unaotumia simu za mikononi.
Matokeo hayo yalitolewa Dar es Salaam
jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Aidan Eyakuze akibainisha kuwa
yanatokana na utafiti uitwao ‘Matarajio na Matokeo, Vipaumbele, Utendaji na
Siasa nchini Tanzania’.
Alisema kuwa idadi kubwa ya wananchi
inaendelea kuukubali utendaji huo licha ya taarifa za kushuka kwa viwango vya
kukubalika kwake, pamoja na vya wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa.
“Huo ni ujumbe mzito wa wananchi
wanaohisi kuwa tofauti na matarajio yao, wameangushwa na utendaji wa Serikali
hii katika kutatua shida zao moja kwa moja,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya hayo wananchi
wanapata hofu na vitu vya msingi kama kipato, chakula na huwa wanatuma ujumbe
mzito kwa viongozi wao.
Alisema utafiti huo unabainisha kuwa
ujumbe mwingine kutoka kwa wananchi ni katika orodha ya matatizo makubwa matatu
yanayowakabili ambayo ni pamoja na afya, elimu na maji ambapo huduma hizo
zimeshuka.
“Sekta hizo kwa miaka mitatu mfululizo
zilichukua nafasi za juu kama changamoto kuu zilizotajwa na wananchi na hivyo
utafiti huu unaashiria kuwa wananchi wanaona mabadiliko katika upatikanaji wa huduma
za jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa matokeo hayo yanatokana
na takwimu zilizokusanywa Aprili kwa wahojiwa 1,805 katika maeneo mbalimbali
Tanzania Bara.
Pamoja na kukubalika kwa Rais Magufuli,
lakini alisema kukubalika kwa viongozi wengine kama wabunge, madiwani na
wenyeviti wa vijiji na wa mitaa kuko chini.
Kwa mfano, kukubalika kwa utendaji wa
wabunge, kumeshuka kutoka asilimia 79 (Juni mwaka jana) hadi asilimia 58
(Aprili).
Kukubalika kwa utendaji wa madiwani,
kumeshuka kutoka asilimia 74 hadi 59 na kukubalika kwa utendaji wa wenyeviti wa
vijiji/mitaa kumeshuka kutoka asilimia 78 hadi 66.
Vyama vya siasa
Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa CCM
imeendelea kuimarika kwa kukubalika kwa kati ya asilimia 54 na 64 kati ya mwaka
2012 na mwaka huu.
“Mwaka 2013 na 2014 kiwango cha
kukubalika kilishuka hadi asilimia 54 kutoka asilimia 65 ya mwaka 2012.
Kukubalika kwa CCM kumeendelea kubaki katika kiwango hicho hicho cha asilimia
62 tangu uchaguzi wa mwaka juzi na asilimia 63 mwaka huu,” ulisema utafiti huo.
Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa
kukubalika kwa Chadema kumeshuka kutoka asilimia 32 mwaka juzi hadi asilimia 17
mwaka huu.
Utafiti huo ulibaini kuwa CCM
inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (80%), ikilinganishwa na asilimia 55 ya
vijana. Wanawake (68%) wanaikubali CCM kuliko wanaume (58%), vijijini (66%)
kuliko mijini (57%), na wananchi masikini (69%) na matajiri (53%).
Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu
ya ufundi au ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46.
Kukubalika kwa Chadema kwa ujumla
kunafuata mtiririko tofauti: ni mkubwa miongoni mwa vijana, wanaume, matajiri
na wenye kiwango kikubwa cha elimu.
0 comments:
Post a Comment