Mwandishi Wetu
Jaji Joseph Warioba |
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba,
ameonya malumbano na kulaumiana yanayoendelea baina ya viongozi kuhusu madini na
rasilimali nyingine za taifa akisema yanaweza kuligawa Taifa.
Aidha, Warioba ambaye alikuwa pia Makamu
wa Kwanza wa Rais amesema yupo tayari iwapo Rais John Magufuli atamhitaji kwa
ajili ya ushauri wenye lengo la kurutubisha sera, sheria na utendaji katika
rasilimali za Taifa kwa faida ya Watanzania wote.
Akizungumza katika mahojiano kwenye ofisi
zake zilizopo Osterbay Dar-es-Salaam kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi na
rasilimali za Taifa, Jaji Warioba alisema ni muhimu sasa viongozi wakaacha
kulaumiana na badala yake waweke kando tofauti zao kwa ajilin ya kutafuta namna
ya kujenga Taifa.
Warioba alisema hayo alipokuwa akijibu
swali lililotaka kujua maoni na mapendekezo yake kwa viongozi wote kuhusu
madini pamoja na Rais John Magufuli kwa hatua zake katika sekta hiyo.
“Naliona hili la malumbano yatatugawa, (viongozi)
waache tofauti zao. Hii lawama ya madini ingekuwa ni mwanzo kwa kuleta mawazo
na maoni ya kutengeneza katika kulinda na kuzitumia rasilimali zote kwa
maendeleo ya Taifa letu,” alisema Warioba na kuongeza:
Jambo la msingi ni kutafuta suluhu
itakayotupeleka mbele, tuone sera zetu zikoje na zinatusaidiaje kulinda
rasilimali za Taifa, tunarekebisha vipi kuondoa tatizo, sheria na utendaji kwa
ujumla. Naomba Watanzania tutoe maoni na mawazo yatakayoboresha sera, sheria na
utendaji au usimamizi wa rasilimali husika. Tunaweza kurudisha miiko na maadili
ya uongozi katika kusimamia rasilimali za nchi, kila Mtanzania ajue sio mali
yake ni ya Watanzania wote, lazima aitunze vinginevyo atahukumiwa kwa hilo.”
Alisisitiza: “Viongozi msaidieni Rais
kulishughulikia kwa pamoja. Hili si jambo la chama wala taasisi. Hakuna haja ya
kupeana lawama, ukishasema tumekosea unatakiwa ueleze tufanye nini, sio kusema Serikali
ichukue hatua, kwani Serikali ni nani, si mimi na wewe. Sasa kwa nini wewe hutaki
kulitolea maoni?”
Akionya na kusisitiza haja kwa viongozi
kuacha malumbano na kulaumiana Warioba alisema: “Tujiamini, nimeona katika
malumbano hayo, wengine wanaonekana kama hatujiamini kama tukifanya hivi
tunaweza kushitakiwa, mabadiliko yoyote yana machungu yake. Tusije tukapoteza
imani tuliyonayo, tunaweza tukapoteza mapato yetu, lakini ni lazima tufanye kwa
kujenga afya ya rasilimali zetu.”
Alisema kutokana na hatua ya Rais kukutana
na mmiliki wa Barick ingawa kila upande una msimamo wake ni vyema kuiachia
suala hilo Serikali na kwamba ni Imani yeke itafanikiwa.
Hata hivyo alisema anashangazwa na
mazungumzo ya baadhi ya viongozi wanaotaka Serikali ihakikishe inazipata
takriban Sh trilioni 108 zilizotajwa kwenye taarifa ya kamati ya Profesa Osoro
akisema mawazo hayo si sahihi.
“Nadhani hili si sahihi, tuna imani na viongozi
wetu wakuu hasa Rais, lolote litakaloafikiwa tulipokee na kulikubali tusije
kuanza kulumbana ripoti imesema trilioni 108 ziko wapi? Pia nilisemee hili la
dalili za kupoteza imani, eti tukifanya hivyo tutashitakiwa sababu ya mikataba
na wawekezaji hawatakuja. Mimi naamini watakuja tu, rasilimali zipo kwetu hawana
jinsi,” alisema Warioba.
Msaada wake kwa Rais
Alipotakiwa kueleza ana msaada gani kwa
Rais Magufuli, Warioba aliyeongoza Tume ta Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba Mpya alisema:
Sisi tupo, Uongozi ni suala la kupeana vijiti, unafika mahali unangatuka watu
wanadhani kungatuka ni kustaafu hapana si sahihi:
Wazee hawaingii katika mambo ya vijana,
sisi tupo lakini hatutaki kuingilia utendaji wao kama sisi tulivyoachiwa
kuendesha nchi, ila Rais akituhitaji tupo tayari kwa ajili ya ushauri anaweza
kuukubali au kuukataa. Nataka nimhakikishie kwa hili tupo pamoja na tutatoa
maoni ya kurutubisha sera, sheria na utendaji katika rasilimali za nchi hii.”
Akizungumzia kauli ya Baba wa Taifa,
hayati Mwalimu Julius Nyerere kutaka madini yaachwe mpaka Watanzania
watakapokuwa na ufahamu wa kutosha ndipo wataamua kuyachimba, Warioba alisema kiongozi
huyo alitoa kauli hiyo baada ya uhuru akiwa hana wataalamu zaidi ya madaktari wawili
na yeye mwenyewe hivyo alikuwa sahihi kwani angeruhusu hilo Watanganyika
wangekuwa watazamaji tu bila kufaidika na lolote.
Akijibu swali lililotaka kujua nini
tatizo kwa Tanzania kuhusu rasilimali na hatua za kuchukua, mwanasiasa na
mbobezi huyo wa sheria alisema haoni kama kuna tatizo la msingi bali ni uelewa
na imani ya watu kwa viongozi.
“Sioni kama kuna tatizo la msingi
lakini, ni suala la uelewa mara nyingi kuna watu ambao huamini viongozi wao kwa
kila kitu wanachosema. Lazima wananchi wawe makini kwa sababu tatizo la Watanzania
ni maendeleo kila mwananchi ana kiu ya kutaka tufikie mahala pazuri kama Taifa
na mimi nakubaliana nao kabisa. Tuna rasilimali nyingi, ambazo kimsingi
tukiweza kuzishughulikia kwa makini kama lilivyoshughulikiwa suala la mchanga
wa madini tutakuwa mbali sana kiuchumi,” alisema.
Akishauri alisema: “Tuangalie rasilimali
ya madini kwa mapana yake na kushughulikia wawekezaji wa ndani na wale wa nje, Barick
na Acaccia ni sehemu ndogo sana ya madini, tuangalie wachimbaji wa ndani, mfano;
Tanzanite ni aibu, madini yanachibwa Manyara biashara hii inatokaje Mererani na
kufanyika Nairobi na New Delhi. Tujiulize kwa nini sio Arusha na Dar-es-Salam?”
Alishauri pia kuangaliwa na kujadiliwa
kwa Taifa linavyoweza kunufaika zaidi na rasilimali zitokanazo na bahari,
maziwa na mito pamoja maliasili za wanayamapori, mbuga za wanyama, vitalu vya
utalii na ardhi.
“Unampaje mfanyabiashara kibali cha
kuwinda miaka 99 yaani atumie yeye, wanawe na wajukuu zake, Watanzania
watatumia lini, haya ni masuala ya msingi kabisa ya kuangalia upya. Lakini tusijidanganye bishara ya madini hata
mafuta ina changamoto kubwa duniani hususan Afrika, biashara hii unapambana na
watu wenye fedha popote utakapokwenda, uchumi unategemea mafuta na madini
utaona jinsi wakubwa wanavyooneemeka na rasilimali hizo na kuwaaacha wananchi
wakiwa masikini, mfano mzuri Nigeria,”alisema Warioba.
Pamoja na kuangalia maadili na nidhamu lazima
kuwe na uwazi katika mikataba ni muhimu sana.
0 comments:
Post a Comment