Abubakari Akida
Wakimbizi kutoka Burundi |
SERIKALI imeahidi kuendelea kutoa huduma
kwa wakimbizi ikishirikiana na mashirika ya ndani na nje ya nchi, huku akiziomba
nchi zenye machafuko kukaa na kutatua changamoto zinazofanya watu kukimbia nchi
zao.
Ahadi hiyo ya Serikali ilitolewa juzi na
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Balozi Ramadhani Mwinyi, alipozungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi
Duniani, iliyofanyika Dar es Salaam.
Balozi Mwinyi alisema Serikali ya
Tanzania imekuwa ikisaidia masuala ya wakimbizi tangu awamu ya Baba wa Taifa na
Rais wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, ikiwamo kuwapa huduma za afya na elimu,
ili kutimiza ndoto zao za kabla ya kukimbia nchi zao.
“Tuunge mkono nguvu ya pamoja
kuhakikisha tunamaliza migogoro kupitia njia ya mazungumzo, ili kumaliza tatizo
la wakimbizi duniani, na tushirikiane na nchi zinazowahifadhi na mashirika ya
kimataifa tukijua kuwa jukumu la kutatua changamoto hii ni letu,” alisema Balozi
Mwinyi
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa
(UN) nchini, Alvaro Rodriguez alisema Umoja wa Mataifa kupitia Shirika lake la
Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lina mkakati maalumu wa kuwahudumia na nchi zinazowahifadhi
(CRRF) kwa lengo la kukabiliana na changamoto za kimaendeleo dhidi ya wakimbizi
katika kambi zao.
Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Chansa
Kapaya alisema Shirika lake litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania
kuhakikisha wakimbizi wanaendelea kupokea misaada ya kibinadamu katika
mazingira yanayowaruhusu kuishi kwa
usalama na hadhi.
Juni 20 dunia huadhimisha Siku ya
Wakimbizi huku ikikadiriwa kuwa kila baada ya sekunde 20 mtu hukimbia nchi yake
na kuacha familia, nyumba na mali kutokana na machafuko, migogoro na uhalifu dhidi
ya binadamu na kundi linaloathirika zaidi ni watoto wanaokadiriwa kuwa wengi kwa
idadi ya wakimbizi milioni 65.6 duniani.
0 comments:
Post a Comment