Wanasiasa wageukia mikataba mikubwa



*Wataka yote yenye utata ielekwe bungeni kujadiliwa
*Wapinzani wataka juhudi za Magufuli ziungwe mkono

Mwandishi Wetu

Rais John Magufuli
WAKATI agizo la Rais John Magufuli kutaka liundwe jopo la kupitia sheria zote za madini na kuzipeleka bungeni ili zipitishwe likisubiri utekelezaji, baadhi ya wanasiasa wametaka mikataba yote mikubwa inayoingiwa na Serikali ipelekwe katika chombo hicho cha kutunga sheria.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti na JAMBO LEO, walisema Taifa limeingia mikataba mingi yenye utata inayoweza kuzua sintofahamu, kama ilivyokuwa kwa mikataba na sheria za madini wakitaka jambo hilo lifanyike mapema ili kukwepa wizi na unyonyaji unaofanywa na baadhi ya wawekezaji.

Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alipokea ripoti ya pili ya Kamati aliyoiunda kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusu mchanga wa madini unaosafirishwa nje, kuagiza kupitiwa kwa sheriza zote za madini na kutaka zipelekwe bungeni, jambo ambalo limepongezwa na watu mbalimbali.

Tayari kampuni ya Acacia ambayo imetajwa katika ripoti hiyo kulitia hasara Taifa ya Sh trilioni 108.06 imekubali kukaa meza moja na Serikali na kufungua njia ya mazungumzo.

Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation ambayo ni mmliki mkubwa wa kampuni ya Acacia, Profesa John Thornton,  juzi alikutana na Rais Magufuli, Ikulu na kukubali kukaa pamoja na Serikali kuzingatia maslahi ya pande zote na kuwa tayari kulipa fedha zote inazopaswa kuilipa Tanzania.

“Suala hapa si mikataba ya madini pekee. Anapaswa kuruhusu mikataba yote yenye maslahi ya nchi ipelekwe bungeni. Katika hili tunamwomba sana Rais kutekeleza, maana tayari ameshaonesha utashi wa kisiasa, anachokipigania ni malengo ya wengi, ikiwemo CCK,” alisema Constatine Akitanda, Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK).

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati hiyo, mikataba ya madini iliyoingiwa  tangu mwaka 1998 ndiyo iliyosababisha upotevu wa kiasi hicho cha fedha,  ambazo zingetumika katika bajeti ya miaka mitatu.

Kwa hali hiyo, ilitoa mapendekezo 21, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua Dk Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo ambao waliwahi kushika nafasi za uwaziri wa nishati na madini kwa vipindi tofauti.

Wengine ni wanasheria wakuu wa zamani na manaibu; Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, Felix Mrema na Sazi Salula.

Wamo pia makamishina wa madini na wakuu wa idara ya mikataba wa zamani; Paulo Masanja, Ally Samaje, Dk Dalaly Kafumu, Maria Ndossi na Julius Malaba.

Katika maelezo yake, Akitanda alisema: “Unakumbuka hapa watu walikunja twiga na kuwasafirisha bila ushahidi kupatikana, tumeona utayari wake, tuko tayari kumsaidia kwani maendeleo ni kwa watu wote, yapo mataifa yanamtukana ila kwa hili lazima Acacia watubu.”

Katibu Mkuu wa chama cha Tanzania Labour (TLP), Nancy Mrikaria alisema ni wakati mwafaka kwa mikataba yote kufika bungeni ili ipitiwe ili kunufaisha wananchi wote.

Alisema Rais Magufuli ameonesha utofauti tangu aingie madarakani, hivyo dhamira yake itaonekana zaidi kama atakubaliana na mapendekezo hayo kwani ni dhahiri mikataba ina changamoto nyingi.

“Ukiwa mpinzani si lazima upinge kila kitu, hivyo kwa hili linapaswa kupongezwa na ndiyo maana tunamshauri aruhusu mikataba yote ipite bungeni ili dhamira ya Rais iweze kuonekana kivitendo,” alisema.

Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju alisema hatua anazochukua Rais kwa sasa ni ishara tosha kuwa ameanza kutekeleza madai ya wapinzani ambao wamekuwa wakililia Katiba mpya ambayo itaonesha aina ya uongozi wa nchi.

“Suala analofanya Rais ni sahihi na lisiishie hapo liende mbali kwa kuhakikisha mikataba kama ya maliasili ambayo inalalamikiwa, ifikishwe bungeni kwa maslahi ya nchi,” alisema.

Alisema kinachohitajika ni haki kutendeka kwa kila upande ambayo itakuwa inahusika katika mabadiliko hayo ili kuepusha mgogoro kwa pande zinazokinzana.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Wananchi (JUKECUF), Severine Mwijage alisema mapendekezo ya Rais ndiyo wamekuwa wakiyapigania miaka yote, hivyo uamuzi huo ni sahihi ila isiwe mikataba hiyo pekee.

Mwijage ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisema yote yanayotokea sasa yanachangiwa na mikataba mibovu, ila kila wakati wamekuwa wakionekana kuwa wanapiga kelele za chura.

Alisema kimsingi suala la uvunjaji mikataba si jambo rahisi, lakini kupitia upya ni hatua muhimu kwa maslahi ya nchi, hivyo ikifika wataipitia ili iendane na hitaji la nchi.

“Mikataba yote ni mibovu hivyo anapaswa kuleta yote kama ana nia ya kusaidia Watanzania kupiga hatua kiuchumi, lakini kama anafanya propaganda hakutakuwa na tija,” alisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu alisema pamoja na kupeleka mikataba bungeni, kinachohitajika ni kuwa na sera moja ambayo inazungumzia uvunwaji wa rasilimali za nchi.

Profesa Baregu alisema pia dhana hiyo itafanikiwa iwapo Katiba mpya hasa ile ya Jaji mstaafu Joseph Warioba ndiyo mkombozi wa rasilimali za nchi.

“Mimi nadhani upo umuhimu wa kuzungumzia sera ya uvunaji rasilimali za nchi upya na hili lipewe nguvu na Katiba kama Watanzania walivyokuwa wamependekeza katika Katiba ya Warioba,” alisema.

Alisema wananchi wamekuwa wakisisitiza uwepo wa sheria ambazo zinatunza na kulinda rasilimali za nchi na kutoa rai kwa wananchi kuachana na dhana ya kushambuliana.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Msafiri Mtemelwa alisema anaamini kila sekta ina udhaifu, hivyo ni vema Rais akaangalia mikataba yote na isiwe ya madini pekee.

“Sisi ACT tumekuwa tukisema ukweli kila mara kuhusu rasilimali za nchi, naamini tukiwa hivyo wote hakuna kitakachoshindikana,” alisema.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo