Nteghenjwa Hoseah, Arusha
WADAIWA sugu wa kodi ya majengo jijini
hapa, watafikishwa mahakamani mwanzoni mwa Julai wakiendelea kukaidi kulipa kodi
hiyo mwisho wa mwaka wa fedha wa 2016/17 unaomalizika Juni 30.
Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo alitoa onyo
hilo kwenye mkutano na waandishi wa habari kukumbusha wananchi kuhusu umuhimu
wa kulipa kodi hiyo mapema kabla ya hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wasiolipa.
Alisema wamiliki wote wa majengo
wanatakiwa kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sharia, lakini hali hairidhishi kwani
wengi wao hawajajitokeza kulipa wakati Serikali inategemea fedha hizo
kutekeleza miradi ya maendeleo.
Aliongeza kuwa muda uliowekwa wa malipo
hayo unaelekea ukingoni ambapo Juni 30 ni mwisho na baada ya hapo, sheria kali zitachukuliwa
kwa watakaobainika kuiibia Serikali kwa kutolipa mapato ya majengo wanayomiliki.
“Haiwezekani unamiliki nyumba halafu
hutaki kuchangia kodi, ninatoa rai wote kulipa kwa hiari, kwa sababu baada ya
hapo ni faini ambayo ni mara tano ya kiasi ambacho ungetakiwa kulipa sasa au
kupelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) wa Mkoa, Apili Mbarouk alisema hadi mwishoni mwa Mei walishakusanya Sh
bilioni moja na siku zilizobaki wanatarajia kukusanya zaidi ya kiwango hicho.
Pia aliongeza kuwa katika maeneo ambayo
hayajapimwa na kufanyiwa uthamini, wamiliki watalipa Sh 15,000 kwa mwaka na kwa
maeneo ambayo yamefanyiwa uthamini wamiliki watalipa kwa kadri ya thamani ya jengo.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara na
wananchi kulipa na kudai risiti kwa kila biashara inayofanyika, ili kuhakikisha
mapato ya Serikali yanakuwa salama na hayapotei.
“Katika hili, tutaanza ukaguzi katika
maeneo yote ya mji huu kuanzia kwa wafanyabiashara na kuhakikisha wanatoa stakabadhi
kwa wateja na ambaye atabainika hajatoa atapigwa faini ya Sh miloini 3 na kwa
mwananchi ambaye atakuwa amenunua bidhaa bila kudai stakabadhi, atatozwa faini
ya Sh 30,000.
Kikao hiki ni mwendelezo ya vikao
maalumu vya kazi anavyofanya Mkuu wa Mkoa pamoja na TRA Mkoa, kuhakikisha
mapato ya Serikali yanakusanywa kwa ufanisi ili kufikia malengo waliyojiwekea.
0 comments:
Post a Comment