Mwandishi Wetu
Mama Samia Suluhu Hassan |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wapelelezi
na waendesha mashitaka nchini kuepuka rushwa na wafanye kazi kwa bidii kwa kutanguliza
maslahi ya nchi kwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya wezi wa rasilimali za
Taifa.
Samia alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati
akizindua mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashitaka wa kesi za wanyamapori.
Taarifa zinaonesha kuwa watuhumiwa 13 wa makosa ya
ujangili wa thamani ya Sh milioni 800 wengi wakiwa wageni waliofikishwa katika
mahakama za Dar es Salaam walitoroka.
Alisema mwongozo aliozindua utasaidia uboreshaji
upelelezi na uendeshaji kesi kuhusu wanyamapori na misitu nchini.
“Uwepo wa mwongozo huu ni dhahiri utatoa matokeo chanya katika
mapambano dhidi ya ujangili na uhalifu wa misitu yetu,” alisema Samia.
Alisema ana imani mwongozo huo utakomesha uhalifu ambao umekuwa
ukiisababishia Serikali hasara kubwa ikiwamo ya uharibifu wa rasilimali za Taifa
na kupoteza mapato ambayo yangesaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini.
Kuhusu sekta ya utalii, Makamu wa Rais alisema pamoja na
sekta hiyo kuliingizia Taifa mapato mazuri, inasikitisha kuona wanyamapori wanazidi
kupungua hivyo kuwa tishio kwa uchumi na nchi.
Alisema ujangili umeendelea kuangamiza wanyama hasa tembo,
hivyo ni muhimu kwa wapelelezi na waendesha mashitaka kutenda haki bila kuonea
mtu kwa wanaokamatwa wakifanya vitendo hivyo ili viweze kukomeshwa nchini.
“Wazee wetu walilinda na kutunza rasilimali zetu kwa faida yetu, nasi
tuzitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema Samia.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe
alimhakikishia Makamu wa Rais kuwa mapambano dhidi ya ujangili na utoroshaji wanyama
na viumbe wengine yatakuwa endelevu na watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali
za kisheria.
Profesa Maghembe alimwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon
Sirro kuendesha oparesheni maalumu ya kukusanya silaha zinazotumika kwa
ujangili ili wanyama hasa tembo wawe salama kwenye maeneo ya hifadhi za Taifa
nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwendesha Mashitaka, Mkuu
wa Serikali, Biswalo Mganga alisema katika kipindi cha mwaka 2014/17 ofisi yake
ilifikisha mahakamani washitakiwa wakubwa wa ujangili ambao wamekuhumiwa
vifungo virefu na faini.
Alisema washitakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya
zaidi ya Sh bilioni 1.1 kwa kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria
na faini hizo zililipwa serikalini.
Alisema katika idadi hiyo, watuhumiwa zaidi ya 80
walihukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 gerezani na faini ya zaidi ya Sh
milioni 164 ambazo bado hazijalipwa serikalini.
Biswalo alisema mafanikio hayo yote yamechangiwa na
usimamizi madhubuti wa kesi hizo kupitia dawati la wanyamapori katika Divisheni
ya Mashitaka na mawakili wa Serikali katika ofisi zote za mikoani.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo
kwenye kazi kwa sasa ni dhamana kwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo vya ujangili
ambapo utafiti unaonesha kuwa mahakama za Dar es Salaam pekee kati ya mwaka
2010 na mwaka juzi 2015 kulikuwa na mashauri 13 yanayohusu nyara za Serikali
zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 800.
Nyara hizo zilikamatwa ndani na nje ya nchi ambapo
watuhumiwa walipewa dhamana na kutoweka.
Biswalo alisema katika mashauri hayo, asilimia 69 ni raia
wa kigeni na asilimia 31 ni wa Tanzania.
0 comments:
Post a Comment