LONDON, Uingereza
Donald Trump |
ZIARA tata nchini ya Rais Donald Trump
wa Marekani, inaonekana kusogezwa mbele hadi mwaka keshokutwa kwa kuwa haikutajwa
kwenye hotuba ya Malkia Elizabeth II.
Ikulu ya White House ya Marekani, ilishakanusha
taarifa kuwa Rais huyo wa Marekani amechelewesha ziara hiyo kutokana na hofu
kwamba itaibua maandamano makubwa kupata kutokea nchini ikipingwa.
Lakini katika hotuba yake bungeni jana,
Malkia hakutaja popote ziara hiyo, ingawa alizungumzia ziara nyingine ya
kitaifa ya Mfalme Felipe na Malkia Letizia wa Hispania mwezi ujao.
Hotuba ya Malkia kwa kawaida hutaja
ziara zote za kitaifa zinazokuja nchini kwa mwaka ufuatao.
Katika hatua isiyo ya kawaida, Serikali
ilisema haitakuwa na hotuba nyingine ya Malkia kwa miaka miwili – ikimaanisha
kwamba ziara ya Trump inaonekana kusogezwa mbele hadi mwaka huo.
Uamuzi wa Waziri Mkuu, Theresa May wa
kutangaza mwaliko wa ziara hiyo ya kitaifa ya Trump haraka vile wakati
akiapishwa, ulisababisha utata.
Angepokewa na Malkia na pengine katika Kasri
la Buckingham na kupewa mapokezi ya heshima zote kama inavyokuwa kwenye
shughuli kama hizo.
Lakini maandamano yalikuwa yametarajiwa
kufanyika jijini hapa, ili kuvuruga ziara hiyo katika kile kilichokuwa
kinatarajiwa kuwa maandamano makubwa ambayo yangesalia kwenye kumbukumbu za
Taifa hili.
Na hasira dhidi ya Trump zimeongezeka wiki
za karibuni baada ya Rais huyo wa Marekani kumshambulia waziwazi Meya wa Jiji
la London, Sadiq Khan kutokana na hatua alizochukua baada ya shambulizi la hivi
karibuni la kigaidi jijini hapa.
Jiji lilikuwa tayari linajiandaa kwa
ghasia kubwa za waandamanaji, huku kukiwa na taarifa kwamba operesheni ya
Polisi peke yake ingeweza kugharimu pauni milioni 10 - na kufanya ziara hiyo
kuwa aghali sana katika historia ya nchi.
Matukio ya waandamanaji wenye hasira mitaani,
yangeongeza shinikizo kwa Waziri Mkuu huyu ambaye ‘ananing’inia kwa uzi’ katika
nyumba Namba 10 baada ya kushindwa kupata kura nyingi kwenye uchaguzi uliopita
wa Bunge.
Wakati huo pia maandamano hayo
yangewaongeza mzigo polisi ambao tayari wanakabiliana na mashambulizi kadhaa ya
kigaidi na njama mbaya zinazopangwa dhidi ya Uingereza.
Na Trump ambaye ni maarufu kwa kukosa
uvumilivu anapokosolewa na umma, angeweza kukasirishwa kwa ziara yake kuvurugwa
na waandamanaji hao.
Ziara ya Mfalme Felipe na mkewe Malkia
Letizia awali ilikuwa imepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi huu, lakini
ikasogezwa mbele ili isigongane na uchaguzi uliofanyika nchini hivi karibuni.
Wawili hao waliojaaliwa mabinti wawili,
watakuwa ni wafalme wa kwanza kutoka Hispania kuja nchini kwa ziara ya kitaifa
tangu mwaka 1986 pale Mfalme Juan Carlos na Malkia Sofia walipokuja hapa. Malkia
Elizabeth II alifanya ziara Hispania mwaka 1988.
0 comments:
Post a Comment