Rais Magufuli ziarani |
Uamuzi wa Rais kufanya ziara hiyo kama
sehemu ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ni wa kutia moyo na hakika
unaamsha ari ya wananchi kuona jinsi kiongozi wao alivyo karibu nao katika
jitihada zake za kuwatafutia maendeleo kwa kuwaondolea adha na kero mbalimbali.
Uzinduzi wa viwanda hivyo, unaweka
uhakika wa wananchi wa maeneo hayo na jirani kupata ajira lakini pia wananchi
wa Pwani na Dar es Salaam wanapata maji safi na salama kwa muda wote na kuwatua
ndoo wanawake.
Rais Magufuli katika ziara hiyo,
anazindua kiwanda cha vifungashio cha Global Packaging Ltd, cha kuunganisha
trekta cha UrsusTamco Ltd, cha chuma cha Kilwa Steel Group, cha matunda cha
Elven Argic na cha vinywaji baridi cha Sayona Fruits.
Wakati anaanza ziara yake wilayani
Kibaha juzi, Rais alitumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wa Kibiti, Mkuranga na
Rufiji dhidi ya watu wachache wanaovuruga amani katika maeneo yao huku
wakiwafahamu bila kuchukua hatua.
Alisema mazingira yaliyo kwenye maeneo
hayo yanazuia wawekezaji kwenda kuwekeza kwa kujenga viwanda vyao, akiwahoji
kuwa nani atakwenda kuwekeza viwanda maeneo ambako watu wanauana? Lakini
akaahidi kukabiliana na waovu hao.
Rais alitoa onyo hilo kutokana na kwamba
katika maeneo hayo kumetokea mauaji ya Watanzania 36 wakiwamo viongozi wa
siasa, Serikali na askari wa Jeshi la Polisi.
Sisi na Watanzania wanaoitakia mema nchi
hii, tunaamini kwamba Rais Magufuli ana nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa
Tanzania inakuwa mahali salama na rafiki ambapo maendeleo yanaweza yakafanyika
na kuonekana.
Kwa maana hiyo, ahadi yake ya
kukabiliana na wavunjifu wa amani Pwani na maeneo mengine nchini ni ya dhati na
ambayo inastahili kuungwa mkono na kila Mtanzania mwema, lakini pia kulinda
miundombinu hiyo ambayo anaizindua.
Tunapenda pia kumsaidia Rais kutoa mwito
kwa wamiliki na wafanyakazi wa miradi hiyo, kuhakikisha wanaitunza ili nao
iwatunze, kwa kuacha kuiba spea za mitambo na bidhaa zinazozalishwa au kwa
kifupi kuacha kuihujumu.
Hiyo ni hatua ya kwanza ya kuelekea
katika kuwa na Tanzania ya Viwanda na ya uchumi wa kati, kamwe hatutafika huko
endapo tutashindwa kuzienzi nguvu na dhamira ya dhati ya Rais Magufuli katika
kuwaletea Watanzania maendeleo.
0 comments:
Post a Comment