Mwandishi Wetu
Dk John Magufuli |
KAULI ya Rais John Magufuli kuwa hataki
kusafiri nje ya nchi kwa sababu akifanya hivyo mambo yataharibika kwani
anaendelea kunyoosha nchi, imeibua hisia tofauti kwa wasomi na wanasiasa.
Baadhi yao wanasema inaweza kuashiria
kutojiamini wengine wakisema inakiuka Katiba huku baadhi wakisema yuko sahihi.
Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara
yake ya siku tatu mkoani Pwani, juzi Rais Magufuli wilayani Kibaha, alisema amepata
mialiko zaidi ya 50 lakini amekataa ili asimamie mipango aliyoahidi kutekeleza
kwa wananchi.
Magufuli alikwenda mbali zaidi na kusema
amesitisha hata posho, semina, warsha na safari kwa watumishi wa umma, kama
hazina tija kwa Taifa, ili kila mtu ajikite kujenga Taifa na kuleta maendeleo.
Akizungumzia kauli hiyo, Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUTI), Profesa Mwesiga Baregu
alisema kauli hizo zinaashiria kuwa Rais Magufuli hajiamini kwa sababu amekuwa
akifanya uamuzi unaokandamiza jamii.
Profesa Baregu alisema katika nchi inayoendeshwa
kwa misingi ya Katiba na demokrasia, Rais hawezi kuhofia kusafiri kwa
kisingizio cha kujenga nchi.
“Mimi nadhani hajiamini, naweza
kuliunganisha hili na kufungia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya hadhara,
kwani kila mtu anaona kinachoendelea nchini, kwa kukandamiza demokrasia,
tunaona madiwani, mameya na viongozi wetu wanavyokamatwa,” alisema.
Aidha, alisema upo uwezekano Rais haamini
watu wa karibu naye na pengine Chadema inampa hofu, kutokana na idadi ya kura
ilizopata kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, hivyo anaongoza kwa kuiweka nchi kwenye
wasiwasi.
Mhadhiri huyo alisema pia uamuzi wake wa
kukaa nchini kwa kisingizio cha kusimamia mipango, inaleta picha ya umimi
katika kila jambo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Shukia alisema anaunga mkono jitihada za Rais
Magufuli katika kusimamia ujenzi wa nchi, lakini akatoa angalizo kuhusu kauli
hizo, akisema zinakiuka Katiba na miongozo ya nchi.
Dk Shukia alisema kwa mujibu wa Katiba,
hakuna kinachoharibika kwa Rais kufanya safari za nje ya nchi kama atakuwa
anaaminiana na wasaidizi wake.
“Mimi naamini anapaswa kujenga imani na
wasaidizi wake na asifike mahali akaona bila yeye hakuna kinachowezekana jambo
ambalo si sawa,” alisema.
Alisema kauli za viongozi zinakwenda
mbali, hivyo Rais anapaswa kuwa makini katika kauli zake na kutambua kuwa urais
ni taasisi si mtu.
“Tunapaswa kuamini kuwa tunafanya kazi
kama familia, naamini hata katika familia, baba akiondoka anatakiwa kuamini
kuwa mambo yatakwenda,” alisema.
Dk Onesmo Kyauke ambaye ni Mhadhiri
Mwandamizi wa UDSM, alisema kauli ya Rais isitafsiriwe kwa ujumla wake, kwa
kuwa amekuwa akisisitiza kwamba anataka kujenga mfumo wa Serikali yake.
“Yeye ndiye mwamuzi wa nani aende nani
asiende, hivyo si lazima aende yeye na kinachohitajika ni alichotakiwa kwenda
kukifanya kimepata mtu au la,” alisema.
Dk Kyauke alisema kwa Tanzania watu wote
wanafanya kazi kwa niaba ya Rais, akitolea mfano wa Waziri Mkuu anayefanya kazi
kwa maagizo ya Rais tofauti na Kenya ambako Naibu Rais anafanya anayotaka kwa
mujibu wa Katiba.
Aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi,
Goodluck ole Medeye alisema Rais amedhamiria kujenga Tanzania anayoitaka, hivyo
katika kutekeleza hilo ni lazima awepo nchini muda wote.
Medeye alisema uamuzi wa Rais Magufuli
ni wa kupongezwa na mpenda maendeleo yeyote na kubainisha kuwa waliokuwa
wamesafiri miaka ya nyuma hakuna jambo la ajabu walilofanya.
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Benson
Bana alisema kilichotokea ni Rais kufanya siasa, hivyo njia rahisi ya
kuwaonesha wapiga kura kuwa yuko nao ni lazima atoe ujumbe aliotoa.
Alisema Rais amekuwa akizungumza kuhusu haiba
ya Tanzania anayoitaka, hivyo kwa utaratibu huo anaofanya anataka
kuwahakikishia kuwa yuko nao katika kupigania mahitaji yao.
“Nadhani alitaka kuonesha kuwa anabana
matumizi ili kujenga Tanzania ya uchumi wa kati na katika hilo dawa ni kuzuia
safari zikiwamo zake,” alisema.
Tangu Rais Magufuli achaguliwe Oktoba 25
na kuapishwa Novemba 5 mwaka juzi amekuwa nchini na alifanya ziara za Rwanda,
Kenya na Uganda jambo ambalo limekuwa
likiibua maswali mengi.
0 comments:
Post a Comment