Wafanyabiashara watakiwa kutii agizo


Seif Mangwangi, Arusha

MKURUGENZI wa Kiwanda cha Usagishaji Nafaka cha Monaban Trading and Farming cha jijini hapa, Dk Philemon Monaban ametaka wafanyabiashara wenzake kutii agizo la Serikali la kutopeleka mahindi nje ya nchi.

Pamoja na kutoa mwito huo, kampuni hiyo pia imetangaza kununua mahindi kwa kiwango cha Sh 600 kwa kilo na hivyo kuwataka wafanyabiashara nchini kupeleka mahindi yao kiwandani hapo.

Dk. Monaban aliwashangaa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakitorosha mahindi nje ya nchi wakati Taifa bado lina uhitaji mkubwa wa mahindi kutokana na janga kubwa la ukame lililolikumba Taifa mwaka jana.

Alisema amelazimika kununua mahindi ili kuunga mkono wakulima na wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilenga masoko ya nje ya nchi huku soko la ndani likiwa halijatosheleza.

"Mimi kuanzia Leo natangaza kununua mahindi, kama kuna wakulima au wafanyabiashara wanapeleka nje ya nchi mahindi, waache waje kiwandani, tutanunua kwa bei nzuri ya Sh 600 kwa kilo," alisema.

Dk Monaban alisema juzi alipokea simu kutoka kwa viongozi wa wilaya za Siha na Rombo mkoani Kilimanjaro, wakimwuliza kama ananunua mahindi baada ya viongozi hao kukamata magari yakisafirisha mahindi nje ya nchi.

"Nilipigiwa simu juzi na wakuu wa wilaya za Siha na Rombo wakiniuliza kama nanunua mahindi, nikawaambia ndio na ndiyo maana unaona hapo nje kuna magari mengi yana mahindi, nanunua mahindi yaliyokamatwa Moshi," alisema.

Alisema Rais Magufuli amekuwa na lengo zuri la kukataza uuzwaji mahindi nje ya nchi ili kutengeneza ajira na kuuza mazao ambayo tayari yamesagwa.

Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo