Suleiman Msuya
Viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania |
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza
kushtushwa, kuhuzunishwa na kushangazwa kwake na hatua ya Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe kulifungia kwa miaka miwili
gazeti la kila wiki la Mawio, adhabu iliyoanza Juni 15, 2017.
Aidha, TEF imesema itaendelea kupinga
vitendo vya uonevu dhidi ya vyombo vya habari ambavyo siyo tu kwamba
vinakandamiza uhuru wa habari, bali vinavunja Sheria inayosimamia sekta ya
habari nchini.
Akitoa tamko la chombo hicho kuhusu
uamuzi wa Waziri Mwakyembe kufungia gazeti hilo jana, Mwenyekiti wa TEF,
Theophil Makunga alisema kitendo cha Serikali kufungia Mawio si sahihi na kwamba
hata sababu zilizoanishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dk. Hassan
Abbasi hazikuwa na tija kwa maslahi ya Taifa.
Makunga alisema kufungia gazeti kutokana
na kuchapisha katika ukurasa wake wa kwanza na ule wa 12 picha na habari
zinazowahusisha marais wastaafu; Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na
usafirishaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi bila kuanisha ni kifungu gani
cha sheria kimevunjwa si sahihi.
Mwenyekiti huyo alisema TEF baada ya
kupitia taarifa ya Serikali ya Juni 15, 2017 iliyotangaza kulifungia Gazeti la
Mawio kwa miaka miwili (2), limebaini Waziri Mwakyembe amekiuka Sheria ya Huduma
za Habari ya 2016 kwa kujivika mamlaka ya Kimahakama ambayo kimsingi hana kwa
mujibu wa sheria hiyo.
“Vifungu vya sheria vilivyotajwa katika
tarifa ya serikali havimpi waziri mamlaka wala wajibu wakufungia chombo
chochote cha habari,” alisema.
Alisema kifungu cha 59 cha Sheria hiyo
kinatoa mamlaka kwa waziri kuzuia maudhui katika habari na siyo kufungia chombo
cha habari kama waziri alivyofanya.
Makunga alisema maudhui yanayopaswa
kuzuiwa na waziri kwa mujibu wa kifungu hicho ni yale yanayohatarisha usalama
wa nchi au usalama wa umma.
Alisema tuhuma kwamba Mawio lilikiuka
vifungu namba 50 (a), (b), (c), (d) na (e) vya Sheria ya Huduma za Habari ya
2016 si za kweli, kwani sehemu hiyo ya sheria inataja makosa ambayo mwandishi
wa habari anaweza kutiwa nayo hatiani ikiwa atafikishwa mbele ya Mahakama.
“Vifungu hivyo vinahitimishwa kwa adhabu
inayotolewa na sheria kwa makosa husika. Adhabu hizo ni faini kati ya Sh.milioni
5 na Sh. milioni 20 au kifungo jela kati ya miaka mitatu na miaka mitano au
vyote kwa pamoja,” alisema.
Alisema makosa yanayotajwa yanaweza
kuthibitishwa tu ikiwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa kuwa waziri siyo
mahakama, hana mamlaka ya kisheria ya kuwatia hatiani Mawio na hawezi kuwa
rejea ya makosa yaliyotajwa katika sheria hiyo.
Aidha, alisema habari katika ukurasa wa
12 wa gazeti la Mawio ambayo inadaiwa kuwa ilichapishwa kinyume cha maagizo na
maelekezo ya serikali, ilinukuu kauli ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),
Tundu Lissu ndani ya Bunge.
Mwenyekiti huyo wa TEF alisema waziri
anapaswa kukumbuka kuwa mijadala ya Bunge na kauli za wabunge ndani ya Bunge ni
miongoni mwa mambo yanayotajwa katika Kifungu cha 38 cha Sheria ya Habari ya
2016 kwamba yanaweza kunukuliwa kama yalivyo bila kujali ukweli au uongo wake.
“Kwa maana hiyo, hatua ya kulifungia
Mawio kwa kuandika taarifa zilizotokana na Bunge, pia ni kukiuka sheria
inayosimamia sekta ya habari,” alisema.
Alisema ni dhahiri kwamba mchakato mzima
wa kulifungia gazeti la Mawio umekiuka Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 ambayo
Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa inalenga kusimamia weledi katika sekta ya
habari.
Alisema TEF inahuzunishwa na utamaduni
uliojengeka miongoni mwa viongozi na watendaji wakuu wa wizara ya habari kwamba
adhabu pekee ya kukimbilia ni kufungia vyombo vya habari.
Alisema uamuzi huo unaondoa dhana nzima
ya malezi na mashauriano na mwenendo huo hauna afya kwa sekta ya habari na nchi
yetu.
Makunga alisema TEF inatoa wito kwa gazeti
la Mawio kutafuta haki yake kama walivyowahi kufanya wakati gazeti hilo lilipofutwa
Januari 2016 na baadaye kurejeshwa na Mahakama.
0 comments:
Post a Comment