Fidelis Butahe
Rais John Magufuli (katikati) |
WAKATI wabunge leo wakitarajiwa kupiga
kura ya wazi kupitisha Bajeti ya mwaka 2017/18 ya Sh trilioni 31.7, Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe ametaja sababu tatu za kuipigia
kura ya hapana bajeti hiyo ya pili ya Rais John Magufuli.
Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema baada
ya siku nane mfululizo za kujadili mapendekezo na makadirio hayo ya Serikali,
bajeti hiyo itapitishwa kwa mbwembwe na wabunge wa CCM, lakini vyama vya
upinzani vitaipinga kwa kile alichokiiita; “haijalenga kumkomboa Mtanzania
masikini.”
Akizungumza na gazeti hili jana, Mbowe
alitaja sababu tatu za wapinzani kuikataa bajeti hiyo kuwa ni; kuongezeka kwa
kiwango cha bajeti kutoendana na maisha halisi ya wananchi, kuongezeka kwa deni
la Taifa na kutokuwa na jibu na suluhisho kwa wananchi juu ya kupanda kwa
gharama za maisha.
Baada ya wabunge kupitisha bajeti kwa
kura ya wazi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango atawasilisha Muswada
wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2017.18 utakaowezesha kutumika kwa fedha hizo.
Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai alitolea
mfano utekelezaji wa asilimia 38 ya bajeti ya mwaka 2016/17 ya Sh trilioni 29
na kuhoji fedha zitakapopatikana kutekeleza bajeti ya Sh trilioni 31.7 walati
vyanzo vya mapato vikiwa havieleweki.
Hata hivyo, Serikali ilieleza sababu
tatu za kutotekelezwa kwa bajeti hiyo kuwa ni; mwenendo wa upatikanaji wa
fedha, upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji na matayarisho hafifu ya miradi
ambayo baadhi imeonekana ama ipitiwe au majadiliano yaanze upya ili kulinda
masilahi ya Taifa.
Bajeti hiyo ya Sh31.7 trilioni
iliyowasilishwa bungeni na Dk Mpango takribani siku 10 zilizopita imeweka
unafuu ambao utasisimua shughuli za kiuchumi baada ya kufanya marekebisho ya
kodi mbalimbali.
Baadhi ya maeneo yaliyowekewa unafuu ni
punguzo la kodi ya usajili wa magari, kufuta Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye
bidhaa za mtaji, huduma za usafirishaji bidhaa kwenda nje, vyakula vya mifumo
na mayai ya kutotoresha vifaranga.
Lakini machungu yatakuwepo katika mafuta
ya petroli, pombe aina ya bia na mvinyo wa nje ambazo kama ilivyo kwa miaka
mingine, zimekuwa zikiongezwa ushuru.
Wakati Serikali ikija na vyanzo vya
mapato vilivyozoeleka, upinzani waliwasilisha bajeti mbadala na kutaja vyanzo
vipya vya mapato ambavyo ni; mapato yatokanayo na uvuvi katika bahari kuu, madini
ya vito kutokana leseni na kodi na malipo kulingana na kipato (P.A.Y.E).
Nyingine ni kupunguza misamaha ya kodi
kwa asilimia moja ya Pato la Taifa, amana za fedha za kigeni (eurobond), mapato
kutoka sekta ya utalii na mapato katika sekta ya michezo ya kubahatisha ambavyo
kwa ujumla wake alisema vingeliingizia Taifa Sh30 trilioni.
Sababu tatu
“Tunaona kama tunapanua wigo mpana wa
bajeti na matumizi makubwa ya Serikali lakini hauendani na kuondoa umasikini wa
Watanzania wa kawaida,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Kukua kwetu kwa Pato la Taifa (GDP)
hakuakisi maisha ya wananchi wa kawaida bali kundi la watu wachache ambao wako
katika sekta muhimu za fedha, ujenzi na mawasiliano.”
Alisema wakati sekta hizo zikimulikwa
zaidi, sekta nyingine kama kilimo, uvuvi na ufugaji ambazo zimeajili asilimia
70 ya Watanzania hazijapwa kipaumbele katika Mpango wa Serikali wa Miaka
Mitano.
Alihoji: “Matokeo yake fedha tunapeleka
kwenye ujenzi wa reli na ununuaji wa ndege. Hata shirika la ndege la Tanzania
linatengewa fedha nyingi kuliko sekta ya kilimo?”
Mbowe ambaye alisema bajeti hiyo huenda
ikawa ya kiini macho zaidi kuliko zote alizozishuhudia tangu awe mbunge miaka
15 iliyopita, alieleza kwamba wapinzani wanaipinga kwa sababu haijaweka msukumo
katika maeneo yanayoweza kunyanyua uchumi wa wananchi.
Kuhusu deni la Taifa ambalo limefikia Sh
trilioni 42.45, Mbowe alisema: “Katika mwaka wa fedha unaokwisha deni la Taifa
lilitumia asilimia 65 ya makusanyo yote ya kodi yatokanayo na TRA (Mamlaka ya
Mapato Tanzania) kukosekana fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.”
“Pamoja na hili Serikali inasema deni
linahimilika na wanaendelea kukopa. Katika mwaka wa fedha unaomalizika Serikali
imekopa Sh trilioni 9 kutoka ndani na nje ya nchi,”alisema.
Kwa mujibu wa Mbowe, katika mwaka ujao
wa fedha (2017/18), fedha itakayolipia deni la Taifa ni kubwa kuliko
iliyotumika kwenye bajeti ya 2016/17.
“Ina maana uwezo wa Tanzania kukusanya
na kupanua mapato unapungua na matumizi ya kuhimili deni la Taifa yanaendelea
kuwa makubwa,” alisema Mbowe.
Alisema kwa mantiki hiyo fedha
zitakazokwenda katika miradi ya maendeleo zitazidi kuwa pungufu ya asilimia
34.6 ya zilizotengwa katika bajeti ya mwaka 2016/17.
“Deni la Taifa linahitaji mkakati maalum
wa kuzuia kukua kwake maana tumeshathibitisha deni hili linatumia makusanyo
mengi ya TRA, tunalazimika kukopa fedha ili kuiendesha Serikali,” alisisitiza.
Akizungumzia kupanga kwa gharama za
maisha alisema wabunge wa CCM wataipitisha bajeti hiyo huku kukiwa hakuna
nyongeza yoyote ya mshahara.
“Kodi imeongezwa katika mafuta na
itaathiri maisha ya wananchi wa kipato cha chini maana kipato chao kipo
palepale. Pia kodi katika vinywaji, sigara na mafuta zitapanda na kuhatarisha
kupanda kwa gharama za maisha kwa wananchi,” alisema.
Mbowe pia aligusia tofauti ya vitabu vya
bajeti ya Serikali, kwamba kitabu cha mapato kinaonyesha kuwa Serikali kwa
mwaka 2017/18 itakusanya Sh trilioni 23.9 wakati kitabu cha matumizi kinasema
watatumia Sh trilioni 26.9 ikiwa ni ongezeko la Sh3 trilioni ambavyo vyanzo
vyake havijaonyeshwa kwenye kitabu cha mapato
Upigaji kura
Akizungumzia upigaji wa kura ya ndio au
hapana, Mbowe alisema tukio hilo ni kama muhuri tu kwa madai kuwa wanahalalishiwa
kitu kilichokwisha hararishwa.
“Kwa utaratibu wa kupiga kura wa wazi
wabunge wa CCM hawawezi kupiga kura ya hapana,” alisema Mbowe na kudai kuwa
wabunge wa CCM walihongwa ili kuikubali bajeti hiyo jambo ambalo lilikanushwa
na viongozi wa chama hicho tawala.
Ndio maana wabunge wa CCM waliishangilia
sana bajeti hii wakati ikiwasilishwa bungeni. Pia nasikitishwa sana na mjadala
wa bajeti kumezwa na ripoti za mchanga wa dhahabu. Watanzania wameshindwa kujua
kasoro za bajeti hii,” alisema Mbowe.
Alifafanua: “Bajeti hii kwanza vitabu
havilingani, vyanzo vya mapato si vya uhakika, vipaumbele si sahihi na
inakwenda kuwakamua zaidi wananchi masikini.”
Alisema kwa kuwa wabunge wa upinzani ni
wachache ndani ya chombo hicho cha dola hawana la kufanya zaidi ya kuwaachia
wananchi kuhakikisha wanachagua wabunge wengi wa upinzani.
Ends
0 comments:
Post a Comment