Celina Mathew
Edward Lowassa |
WAZIRI Mkuu wa zamani ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, Edward Lowassa amehojiwa kwa zaidi ya saa nne na Mkurugenzi wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai
(DCI), Robert Boaz.
Sababu za DCI kumhoji Lowassa ni baada ya kudaiwa kuwa
ametoa kauli ya uchochezi baada ya kutaka Rais John Magufuli kutafakari hatima
ya masheikh wa Jumuia ya Uamsho na mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki)
maarufu ëUamshoà wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.
Hivyo kutokana na kauli hiyo ambayo Lowassa aliitoa siku za
karibuni, juzi Jeshi la Polisi Makao Makuu lilitoa taarifa kuwa anahitajika kwa
DCI kwa ajili ya kuhojiwa na jana alitii agizo hilo na kwenda kuhojiwa.
Akizungumza jana baada ya Lowassa kuhojiwa na DCI, Wakili
wake, Peter Kibatala alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani alipomaliza kuhojiwa
alijidhamini mwenyewe ila kesho atatakiwa kwenda tena kwa ajili ya mahojiano
mengine.
Wakili Kibatala alisema kwa mujibu wa mahojiano hayo,
Lowassa anadaiwa kutoa matamshi hayo siku tatu zilizopita katika futari
iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga jijini Dar es Salaam, Mwita Waitara (Chadema).
Lowassa ataja kiini cha kuhojiwa Akizungumza na waandishi
wa habari kutoka vyombo mbalimbali nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam,
Lowassa alisema ameitwa kuhojiwa Polisi kutokana na hotuba yake aliyotoa kwenye
futari.
“Watu wametafsiri ni uchochezi. Nimewajibu na wanaendelea
kutafakari. Tunakutana tena Alhamisi (kesho) saa sita mchana. Siwezi kueleza
tumezungumza nini. Nawataka tu watu kuwa watulivu katika kipindi hiki,” alisema
Lowassa.
Hata hivyo, Lowassa ambaye hakutaka kujibu baadhi ya
maswali kutokana na kile alichokiita kuingilia mahojiano hayo aliwashukuru
wanahabari kwa kuandika habari mbalimbali za kuisaidia nchi huku akifafanua kuhojiwa
si jambo baya na kutaka hatua stahiki zizingatiwe.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Vicent Mashinji alipoulizwa
kuhusu kitendo cha Lowassa kuhojiwa, alisema alichokisema Lowassa kuhusu Uamsho
wanaungana nacho kwani ni kweli mashekhe hao wamekaa rumande kwa muda mrefu.
Dk. Mashinji ambaye alionekana akizuiwa kwa nyakati
tofauti na Lowassa kutozungumza kwa undani suala hilo, alisema hata Katiba ya
nchi inampa mshtakiwa uhuru hadi pale mashtaka dhidi yake yatakapothibitishwa.
Kauli ya Lowassa katika futari Lowassa, alisema ni jambo
la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu
viongozi wa dini (mashekhe) muda mrefu kiasi hicho bila kesi kusikilizwa
mahakamani.
Kwa kukumbusha tu mashekhe hao awali walikuwa
wamefunguliwa kesi ya ugaidi, ambayo ilikuwa ikiendeshwa Mahakama Kuu ya
Zanzibar na baadaye kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es
Salaam inakoendelea hadi sasa.
Hivyo Lowassa alisema iwapo mashekhe hao wamefanya makosa
wapelekwe mahakamani ili haki itendeke lakini kuendelea kuwashikilia ni fedheha
kubwa kwa Taifa.
Lowassa alisema kama ambavyo Rais John Magufuli
ametekeleza ahadi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa
kuunda tume mbili za kushughulikia madini ya dhahabu, hana budi kutekeleza na
ahadi yake (Lowassa) kuwatoa kizuizini mashekhe hao wa Uamsho.
Uamsho mwaka 2011 Mwaka 2011 viongozi hao wa Uamsho
wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) walikamatwa na kufunguliwa mashitaka
kwa tuhuma za kusababisha uharibifu wa mali za watu na Serikali na kuhatarisha usalama
wa taifa.
Mara kadhaa wamekuwa wakifikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto
kutokana na kushitakiwa kwa tuhuma za ugaidi.
Mbali na kina Farid, kesi za ugaidi zaidi ya 20
zinaendelea mahakamani zikiwahusisha washtakiwa zaidi ya 60.
0 comments:
Post a Comment