Paul Wilium, Moshi
Moshi, Kilimanjaro |
HALI ya taharuki imeibuka katika Halmashauri ya Moshi
baada ya madiwani kugomea mafunzo ya utaratibu ulioboreshwa wa uendeshaji ruzuku ya maendeleo kwenye mamlaka za
Serikali za mitaa (LGDG), wakishinikiza kulipwa posho ya Sh 100,000 kila
mmoja.
Mafunzo hayo yaliyokuwa yanasimamiwa na Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), yalihusisha madiwani wote na
wakuu wa idara jana katika ofisi za Halmashauri.
Taharuki iliibuka baada ya madiwani hao kuingia ukumbini na
kabla ya mafunzo kuanza, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Michael Kilawila aliwatangazia kuwa kutokana na mafunzo
kutokuwa ya kisheria, Halmashauri itapaswa kutoa posho zao kupitia makusanyo ya
ndani.
Kilawila alisema
kutokana na hali hiyo na mapato kuwa madogo, kila diwani atalipwa Sh elfu
60,000 kama posho ya siku moja ambapo siku mbili za mafunzo hayo kila mmoja
angepokea Sh 120,000.
Baada ya tamko hilo
hali iligeuka baada ya madiwani hao kuonesha kutoridhishwa na kiwango hicho cha
posho na kugonga meza wakishinikiza kulipwa Sh 100,000 kwa siku kama
wanavyolipwa kwa vikao vingine vinavyotambulika.
Waliposhindwa
kuelewana, madiwani hao walisusia mafunzo hayo na kuondoka hali iliyowalazimu
wakufunzi kutoka Tamisemi kufundisha wakuu wa idara peke yao.
Akizungumzia sintofahamu
hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Butamo Ndalahwa alisema lengo la
mafunzo hayo ni kuhakikisha madiwani kwa kushirikiana na wananchi, wanaibua
miradi.
Ndalahwa alisema mafunzo hayo yanafanyika katika halmashauri
zote nchini na kuwa madiwani hao waligoma wakitaka posho kubwa bila kujali kuwa
mafunzo hayo yangenufaisha wananchia ambao ndio waliowachagua.
Mkurugenzi huyo akionesha masikitiko, alisema jambo hilo
la kugomea mafunzo litasababisha maendeleo ya Halmashauri kurudi nyuma kwa
kukosa elimu ya uibuaji miradi ambayo inakubalika.
“Nimesikitishwa kwa kiasi kikubwa, madiwani wameonesha kutangulia
mbele maslahi yao badala ya kutumikia wananchi waliowachagua, tumewaelimisha
kuhusu posho, kwa nini tunawapa Sh 60,000 lakini hawakutaka kuelewa na badala
yake waligonga meza ovyo na kutoka nje,” alisema Ndalahwa.
Kilawila alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia suala
hilo na hatima yake, alisema hawezi kuzungumzia jambo lolote mpaka kikao cha
madiwani kitakapokaa ili kutoa maazimio.
“Ninachoweza kusema sasa ni kwamba siwezi kuzungumza lolote,
mtafute Mkurugenzi, mimi nasubiri ni
kikao cha madiwani ili kutoa maazimio ya kilichotokea leo,” alisema Kilawila.
0 comments:
Post a Comment