Venance Matinya, Mbeya
ILI kupunguza maambukizi mapya ya virusi
vya Ukimwi na magonjwa ya njia ya mkojo mkoani Songwe, zaidi ya wanaume 26,556
wanatarajiwa kufanyiwa tohara kwa mwaka huu.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni
ya kuhamasisha tohara kwa wanaume mkoani humo kwenye viwanja vya shule ya
msingi ya Tunduma, Mshauri wa Ufundi wa Tohara (WRP) wa Kanda ya Nyanda za Juu
Kusini, Dk Zegeli Balishanga alisema wizara kwa kushirikiana na wadau HJFMRI
imeandaa kampeni ya siku 28 ili kufikia malengo ya kutahiri wanaume hao.
Alisema imebainika kuwa Songwe na Mbeya iko
kwenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia tisa kutokana na
wanaume wengi kutotahiriwa, hivyo kuambukizwa kirahisi na kuambukiza wenzao.
Aliongeza kuwa tohara inasaidia kumkinga
mwanamume dhidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60 hivyo
itasaidia kupunguza idadi ya waathirika wa Ukimwi na kupunguza uwezekano wa
kupata magonjwa ya zinaa, kukinga saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake na saratani
ya uume.
Alizitaja faida zingine kuwa ni
kupunguza magonjwa ya njia ya mkojo kwa wanaume, kurahisisha usafi na kumfanya
mwanamume kujiamini zaidi kuliko kuishi bila tohara, hususani akiwa na umri
mkubwa.
Innocent Ndunguru, Mratibu wa WRP wa Mkoa
wa Songwe, alisema ili kufikia malengo, mkoa umetenga vituo vinane vya tohara
ambavyo ni hospitali ya Misheni ya Mbozi, zahanati za Nyimbili, Namabinzo, Ihanda,
Myunga, Mkulwe, Chitete na Magamba.
Alisema kampeni hiyo yenye kaulimbiu ya ‘Amka
sasa, Wahi tohara, kuwa msafi, pata kinga’, inalenga jamii kupata ujumbe ili
kufahamu umuhimu wa tohara katika kupambana na maambukizi.
Aliongeza kuwa kampeni hiyo inalenga kutahiri
wanaume 13,911 sawa na asilimia 52 ya malengo yaliyotolewa na Serikali kwa mwaka
kwa Songwe ambako kuna mwitikio mkubwa uliofanya wanaume 11,286 sawa na
asilimia 81 kutahiriwa ndani ya muda wa kampeni.
Nao watoa huduma za tohara, Neema
Mahenge na Wilson Kasanga walisema wanaume wengi walijitokeza huku wengine
wakisindikizwa na wenza wao.
“Wengi wanakuja na watoto na wajukuu zao
na hutahiriwa kwa pamoja bila woga na wachache wanasindikizwa na wenza wao,
ambao wako kwenye uhusiano wakitarajia kufunga ndoa jambo linaloashiria elimu
kuwafikia vizuri,” alisema Kasanga.
Waliongeza kuwa changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo ni imani potofu kwa baadhi ya jamii ambazo zimekuwa zikidai
kuwa ngozi iliyokatwa baada ya tohara hutaka waizike jirani na nyumbani kwao
jambo linalowasababishia usumbufu.
Awali mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa kampeni
hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Momba, Juma Irando kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe,
Chiku Galawa alitoa mwito kwa jamii na wananchi kujitokeza kwa wingi kufanyiwa
tohara bure.
Aidha, alitoa mwito kwa watoa huduma
kuongeza kasi na ufanisi wa kazi hiyo ili kuendana na mwitikio mzuri wa
wananchi waliokubali kufanyiwa tohara kwa hiari yao.
0 comments:
Post a Comment