Adaiwa kukutwa na suruali 5,000 za JWTZ


Grace Gurisha

MFANYABIASHARA Casto Ngogo (35), amepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na vifaa vya Serikali ambavyo ni suruali 5,000 za sare ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Ngogo ambaye ni mkazi wa Tabata, Segerea, Dar es Salaam alifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa kusomewa mashitaka yanayomkabili.

Wakili wa Serikali, Hamisi Saidi alidai kuwa Juni 15, maeneo ya Bandari Kavu ya Galco, Chang'ombe, Temeke, Dar es Salaam, Ngogo alikutwa na suruali hizo 5,000 za JWTZ kwenye kontena namba PCIU 82851 (5) zikiwa na thamani ya Sh milioni 59 mali ya Serikali bila  kibali.

Baada ya kusomewa mashitaka, Ngogo alikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na hauna pingamizi na dhamana.

Hakimu Nongwa alisema ili mshitakiwa awe nje kwa dhamana anatakiwa awe na fedha taslimu Sh milioni 30 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo na wadhamini wawili watakaosaini dhamana ya Sh milioni 10 kila mmoja.

Ngogo alitimiza masharti hayo na kuachwa huru na kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 17 itakapotajwa.    
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo