Ziara ya Trump Uingereza kizungumkuti


LONDON, Uingereza

Donald Trump
ZIARA tata nchini ya Rais Donald Trump wa Marekani, inaonekana kusogezwa mbele hadi mwaka keshokutwa kwa kuwa haikutajwa kwenye hotuba ya Malkia Elizabeth II.

Ikulu ya White House ya Marekani, ilishakanusha taarifa kuwa Rais huyo wa Marekani amechelewesha ziara hiyo kutokana na hofu kwamba itaibua maandamano makubwa kupata kutokea nchini ikipingwa.

Lakini katika hotuba yake bungeni jana, Malkia hakutaja popote ziara hiyo, ingawa alizungumzia ziara nyingine ya kitaifa ya Mfalme Felipe na Malkia Letizia wa Hispania mwezi ujao.

Hotuba ya Malkia kwa kawaida hutaja ziara zote za kitaifa zinazokuja nchini kwa mwaka ufuatao.

Katika hatua isiyo ya kawaida, Serikali ilisema haitakuwa na hotuba nyingine ya Malkia kwa miaka miwili – ikimaanisha kwamba ziara ya Trump inaonekana kusogezwa mbele hadi mwaka huo.

Uamuzi wa Waziri Mkuu, Theresa May wa kutangaza mwaliko wa ziara hiyo ya kitaifa ya Trump haraka vile wakati akiapishwa, ulisababisha utata.

Angepokewa na Malkia na pengine katika Kasri la Buckingham na kupewa mapokezi ya heshima zote kama inavyokuwa kwenye shughuli kama hizo.

Lakini maandamano yalikuwa yametarajiwa kufanyika jijini hapa, ili kuvuruga ziara hiyo katika kile kilichokuwa kinatarajiwa kuwa maandamano makubwa ambayo yangesalia kwenye kumbukumbu za Taifa hili.

Na hasira dhidi ya Trump zimeongezeka wiki za karibuni baada ya Rais huyo wa Marekani kumshambulia waziwazi Meya wa Jiji la London, Sadiq Khan kutokana na hatua alizochukua baada ya shambulizi la hivi karibuni la kigaidi jijini hapa.

Jiji lilikuwa tayari linajiandaa kwa ghasia kubwa za waandamanaji, huku kukiwa na taarifa kwamba operesheni ya Polisi peke yake ingeweza kugharimu pauni milioni 10 - na kufanya ziara hiyo kuwa aghali sana katika historia ya nchi.

Matukio ya waandamanaji wenye hasira mitaani, yangeongeza shinikizo kwa Waziri Mkuu huyu ambaye ‘ananing’inia kwa uzi’ katika nyumba Namba 10 baada ya kushindwa kupata kura nyingi kwenye uchaguzi uliopita wa Bunge.

Wakati huo pia maandamano hayo yangewaongeza mzigo polisi ambao tayari wanakabiliana na mashambulizi kadhaa ya kigaidi na njama mbaya zinazopangwa dhidi ya Uingereza.

Na Trump ambaye ni maarufu kwa kukosa uvumilivu anapokosolewa na umma, angeweza kukasirishwa kwa ziara yake kuvurugwa na waandamanaji hao.

Ziara ya Mfalme Felipe na mkewe Malkia Letizia awali ilikuwa imepangwa kufanyika mwanzoni mwa mwezi huu, lakini ikasogezwa mbele ili isigongane na uchaguzi uliofanyika nchini hivi karibuni.

Wawili hao waliojaaliwa mabinti wawili, watakuwa ni wafalme wa kwanza kutoka Hispania kuja nchini kwa ziara ya kitaifa tangu mwaka 1986 pale Mfalme Juan Carlos na Malkia Sofia walipokuja hapa. Malkia Elizabeth II alifanya ziara Hispania mwaka 1988. 
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo