Wananchi waomba kuhifadhi mazingira


Dalila Sharif

Wilaya ya Temeke
WAKAZI wa wilaya za Temeke na Kigamboni wameiomba Wakala wa Huduma za Misitu (TSF) kuwashirikisha kwa kuwapa elimu ya utunzaji  mazingira ili kunufaika nayo katika kulinda mazao yake, kuzuia uchomaji mkaa na ukataji miti ovyo.

Wakizungumza Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti, wananchi hao walieleza wanavyotambua wajibu wao katika utunzaji mazingira.

Mmoja wa wakazi hao kutoka Temeke, Mariam Swedi alisema ni wajibu wa kila mwananchi kushirikishwa katika utunzaji mazingira ya misitu kama mazao, uoto wa asili, nyuki, bustani na aina zingine.

“Hali hii imejitokeza kwa baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam kukosa mwamko wa kushirikishwa katika utunzaji na ulinzi wa misitu yetu hivyo kusababisha wachache kunufaika nayo kwa uvunaji holela wa mazao ya misitu,” alisema Mariam.

Mkazi wa Kigamboni, Burhani Kambi alisema zipo baadhi ya sehemu wananchi hunufaika na mazao ya misitu hivyo hushirikisha wananchi ni jambo la msingi ili kuilinda na kuitunza, wavunaji haramu wasivamie na kuiba mazao na kukata kuni au kuchoma mkaa.

“Kwa nini wananchi tunaoishi mijini hatushirikishwi kulinda na kuitunza hata kunufaika nayo hali ambayo inabaki kusimamiwa na mawakala wa misitu pekee; watushirikishe nasi tunaweza kuiendeleza kama vijijini ambako wananchi wanajumuika kuitunza na kuwaingizia mapato,” alisema Kambi.

Pamela Oscar wa Kigamboni alisema ingawa wilaya hiyo imejaaliwa neema ya misitu kama wa Mwandege, wananchi wanastahili elimu ya juu ya umuhimu wa misitu na kuacha uharibifu wa ukataji miti ovyo pembezoni mwa wilaya hizo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo