Acacia yakubali kuilipa Tanzania


*JPM akutana Ikulu na Mwenyekiti wa Barrick
*Timu yake na ya Tanzania kukaa kujadiliana

Suleiman Msuya

Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amesema kampuni Barrick Gold Corporation imekubali kulipa fedha zitakazobainika kuwa inadaiwa kutokana na uchimbaji madini wanaofanya nchini, baada ya mazungumzo.

Alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya kuzungumza na Mwenyekiti wa Barrick yenye asilimia 64 ya hisa za Acacia, Profesa John Thornton aliyefuatana na Balozi wa Canada nchini, Ian Myles wakimshirikisha Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi.

Profesa Thornton alikuja nchini siku tatu baada ya Kamati Maalumu ya Kuchunguza Masuala ya Kisheria na Kiuchumi kuhusu mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya nchi kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Magufuli ikionesha Taifa kupata hasara.

Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe wanane wakiongozwa na Profesa Nehemiah Osoro, wengine wakiwa ni Profesa Longinus Rutasitara, Dk Oswald Mashindano, Gabriel Malata, Casmir Kyuki, Butamo Kasuka, Usaje Asubisye na Andrew Massawe.

Kwa mujibu wa ripoti yake, Kamati hiyo ilibainisha kuwa mikataba ya madini tangu mwaka 1998 ndiyo ililisababishia Taifa upotevu wa takriban Sh trilioni 108.46 ambazo zingetumika kwenye bajeti ya miaka mitatu kwa kuakisi bajeti ya mwaka 2017/18 huku baadhi ya mawaziri na wanasheria wakitajwa kushiriki kuikosesha Serikali mapato hayo.

Akizungumza baada ya mazungumzo hayo, Rais Magufuli alisema mazungumzo yao yalikwenda vizuri na Mwenyekiti huyo wa Barrick aliridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa na Serikali.

Rais Magufuli alisema Barrick italeta timu itakayofanya kazi na timu ya Tanzania kupitia ripoti zote ili kufikia mwafaka.

“Wameridhika na juhudi tulizofanya kama Serikali na kuwa wamesikia kilichofanywa, lakini ataleta timu yake ili kupitia mapendelezo na timu yetu,” alisema na kuongeza:

“Profesa Thornton amekubali chochote kitakachokubalika watalipa, uzuri alikuwepo Profesa Kabudi, mwanasheria. Nikafurahi nikasema hawa ni wanaume, lakini pia wakasema ni bahati mbaya, wanatubu kwa yalitokea.”

Rais Magufuli alisema Serikali inakaribisha mazungumzo baina ya pande hizo na itaunda jopo la wataalamu watakaofanya majadiliano na Barrick, ili kufikia makubaliano ya kulipwa fedha zinazodaiwa na namna kampuni hiyo itakavyoendesha shughuli zake nchini kwa maslahi ya pande zote mbili.

Alisema pamoja na kukubali kulipa fedha inazodaiwa, Profesa Thornton alikubali kushirikiana na Tanzania kujenga mtambo wa kuchenjulia dhahabu nchini.

Profesa Thornton alisema walikuwa na majadiliano mazuri yatakayowafikisha mahali ambapo kila mmoja atafaidika na uwekezaji huo.

“Nimekuja hapa kuzungumza kuhusu yanayowasibu Acacia, ili tuweze kufikia mwafaka na nimemwahidi Rais kuwa tutakuwa na mazungumzo mazuri ambapo kila mtu atafaidika, hivyo timu zetu zitakutana mapema iwezekanavyo,” alisema.

Kamati ya Pili ya Rais Magufuli ilitoa mapendekezo 21 kwa Serikali ikiwamo kutaka mawaziri waliohusika na mikataba hiyo kuanzia mwaka 1998, wanasheria wakuu na manaibu wao na watumishi wa wizara wahojiwe ili ukweli ujulikane.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo