Askofu: JPM ni mwanamume


*Ni kwa juhudi zake za kupigania rasilimali za nchi

*Amwombea ushirikiano ili Watanzania wale siagi kama Wazungu

Seif Mangwangi, Arusha

Rais John Magufuli akiwa bandarini
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la International Evangelism Church (IEC), Sakila la Arumeru jijini hapa, Dk Eliud Issangya amemwelezea Rais John Magufuli, kuwa ‘mwanamume shujaa na mzalendo’ kutokana na hatua anazochukua za kupigania rasilimali za Tanzania.

Akizungumza jana jijini hapa, Askofu Issangya alisema Kanisa lake linampongeza Rais Magufuli kwa kuzuia usafirishaji mchanga wa dhahabu na kumtaka kuhamishia mapambano hayo kwa wabadhirifu wa rasilimali za nchi katika sekta za wanyamapori, mafuta na gesi.

Alisema sekta za wanyamapori, mafuta na gesi hazina tofauti na sekta ya madini, hivyo Rais hana budi kufuatilia nyendo katika sekta hizo na kuzuia wizi unaoendelea kufanywa kwa miaka mingi sasa.

“Ni miaka miwili sasa, tangu Rais Magufuli achaguliwe, lakini ameonesha yeye ni mzalendo namba moja na shujaa wa kupigania rasilimali za Tanzania.

“Kaonesha ulimwengu kuwa rasilimali hizo ni za Watanzania na si za Wazungu, sisi tunakupongeza Rais, wewe ni mwanamume, hakika umethubutu,” alisema Askofu Issangya.

Alisema Dk Magufuli ni kiongozi anayestahili kuigwa na kutoa mwito kwa Watanzania kuungana kumwombea afya njema, ili afanikishe malengo aaliyojiwekea ikiwamo kuzuia wizi wa rasilimali za nchi.

Askofu Issangya alisema uzalendo anaoonesha Dk Magufuli hivi sasa, kwa miaka ijayo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi tajiri duniani na bei ya vitu muhimu kama vyakula na mafuta itashuka.

“Rais akiendelea na kasi hii hii, kama Kanisa tunaamini umasikini utakwisha kabisa na kwanza umeshaanza kwisha, kila Mtanzania atakula siagi kama Wazungu wanavyokula na hii ni kwa sababu Rais ameamua kusema basi imetosha,” alisema.

Aliwataka wapinzani kuungana na Rais na kuacha kupinga juhudi alizoanzisha, kwa kuwa kufanya hivyo ni kumkatisha tamaa na matokeo yake ni kurudisha nyuma jitihada anazofanya na kulifanya Taifa kuendelea kuwa masikini licha ya utajiri uliopo.

Katika hatua nyingine, Askofu Issangya alimwomba Rais kuwapa wachimbaji wadogo maeneo, ili kupunguza migogoro ambayo imekuwa ikishuhudiwa kutokea mara kwa mara wakigombana na wachimbaji wakubwa.

Askofu Issangya katika kikao hicho alifuatana na msaidizi wake, Mchungaji Gabriel Maasa, Askofu Gerald Mollel wa IEC Kilimanjaro Magharibi na Askofu Michael Laizer wa Arusha Mashariki. Pia aliwapongeza wasaidizi wa Rais; Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo