Ushahidi dhidi ya kina Kitilya watoka Uingereza


Grace Gurisha

Kitilya na wenzake
UPANDE wa mashitaka, katika kesi inayomkabili aliyekuwa Kamishna Mkuu  wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa wamepokea awamu ya kwanza ya vielelezo vya upelelezi kutoka Uingereza.

Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha wa Mahakama hiyo wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Msigwa alidai kuwa bado wanasubiri awamu ya pili ya vielelezo na kwamba wanatarajia vitafika wakati wowote kuanzia sasa.

Baada ya kudai hivyo, Wakili wa utetezi, Mwanahamisi Adam aliomba upande wa mashitaka ueleze muda mwafaka utakaotumika vielelezo hivyo kufika nchini.

Hakimu Mkeha alisema huo muda uliotajwa na upande wa mashitaka uwe ndani ya simu 14 na ikishindikana Juni 30 waeleze vitafika ndani ya siku ngapi.

Mbali ya Kitilya, wengine ni mshindi wa Mashindano ya Urembo mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa kati ya Machi 2013 na Septemba mwaka juzi, wakati wa mchakato wa mkopo wa dola milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania kutoka benki ya Standard ya Uingereza.

Washitakiwa hao wanadaiwa kula njama na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kutakatisha fedha.

Sinare katika kesi hiyo, anadaiwa  kuwa  Agosti 2, 2012 alighushi kwenye makao makuu ya benki ya Stanbic, Kinondoni kwa  nia ya kudanganya ambapo aliandaa nyaraka za mapendekezo akijaribu kuonesha kuwa Standard ikishirikiana na Stanbic wangetoa mkopo wa dola milioni  550 kwa Tanzania kwa ajili ya ada ya uwezeshaji ya asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo, wakati akijua kuwa si kweli.

Inadaiwa kuwa Agosti 2, 2012, Sinare alitoa nyaraka za uongo za mapendekezo kuonesha kuwa Standard ikishirikiana na Stanbic  wangetoa mkopo wa dola milioni  550 na kuziwasilisha kwenye ofisi za Hazina  wakati akijua kuwa si kweli.

Pia anadaiwa kuwa Septemba 20, 2012 katika  makao makuu ya  Stanbic, Kinondoni, alighushi barua ya mapendekezo ikionesha kuwa Standard ikishirikiana na Stanbic  wangetoa mkopo wa dola milioni  550 kwa Tanzania  kama ada ya uwezeshaji wa asilimia 2.4 ya kiasi cha mkopo huo wakati akijua kuwa si kweli.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo