Utendaji wa JPM wakubalika kwa 71%


Mwandishi Wetu

UTAFITI uliofanywa na taasisi ya Twaweza umebaini kuwa asilimia 71 ya Watanzania wanaukubali utendaji kazi wa Rais John Magufuli ingawa kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 96 ikilinganishwa na ulipofanyika Juni mwaka jana.

Utafiti huo unatokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.

Matokeo hayo yalitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Aidan Eyakuze akibainisha kuwa yanatokana na utafiti uitwao ‘Matarajio na Matokeo, Vipaumbele, Utendaji na Siasa nchini Tanzania’.

Alisema kuwa idadi kubwa ya wananchi inaendelea kuukubali utendaji huo licha ya taarifa za kushuka kwa viwango vya kukubalika kwake, pamoja na vya wabunge, madiwani na wenyeviti wa mitaa.

“Huo ni ujumbe mzito wa wananchi wanaohisi kuwa tofauti na matarajio yao, wameangushwa na utendaji wa Serikali hii katika kutatua shida zao moja kwa moja,” alisema.

Aliongeza kuwa licha ya hayo wananchi wanapata hofu na vitu vya msingi kama kipato, chakula na huwa wanatuma ujumbe mzito kwa viongozi wao.

Alisema utafiti huo unabainisha kuwa ujumbe mwingine kutoka kwa wananchi ni katika orodha ya matatizo makubwa matatu yanayowakabili ambayo ni pamoja na afya, elimu na maji ambapo huduma hizo zimeshuka.

“Sekta hizo kwa miaka mitatu mfululizo zilichukua nafasi za juu kama changamoto kuu zilizotajwa na wananchi na hivyo utafiti huu unaashiria kuwa wananchi wanaona mabadiliko katika upatikanaji wa huduma za jamii,” alisema.

Aliongeza kuwa matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa Aprili kwa wahojiwa 1,805 katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara.

Pamoja na kukubalika kwa Rais Magufuli, lakini alisema kukubalika kwa viongozi wengine kama wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji na wa mitaa kuko chini.

Kwa mfano, kukubalika kwa utendaji wa wabunge, kumeshuka kutoka asilimia 79 (Juni mwaka jana) hadi asilimia 58 (Aprili).

Kukubalika kwa utendaji wa madiwani, kumeshuka kutoka asilimia 74 hadi 59 na kukubalika kwa utendaji wa wenyeviti wa vijiji/mitaa kumeshuka kutoka asilimia 78 hadi 66.

Vyama vya siasa

Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa CCM imeendelea kuimarika kwa kukubalika kwa kati ya asilimia 54 na 64 kati ya mwaka 2012 na mwaka huu.

“Mwaka 2013 na 2014 kiwango cha kukubalika kilishuka hadi asilimia 54 kutoka asilimia 65 ya mwaka 2012. Kukubalika kwa CCM kumeendelea kubaki katika kiwango hicho hicho cha asilimia 62 tangu uchaguzi wa mwaka juzi na asilimia 63 mwaka huu,” ulisema utafiti huo.

Kadhalika utafiti huo ulibaini kuwa kukubalika kwa Chadema kumeshuka kutoka asilimia 32 mwaka juzi hadi asilimia 17 mwaka huu.

Utafiti huo ulibaini kuwa CCM inakubalika zaidi miongoni mwa wazee (80%), ikilinganishwa na asilimia 55 ya vijana. Wanawake (68%) wanaikubali CCM kuliko wanaume (58%), vijijini (66%) kuliko mijini (57%), na wananchi masikini (69%) na matajiri (53%).

Wananchi wenye elimu ya sekondari, elimu ya ufundi au ya juu wanaikubali CCM kwa asilimia 46.

Kukubalika kwa Chadema kwa ujumla kunafuata mtiririko tofauti: ni mkubwa miongoni mwa vijana, wanaume, matajiri na wenye kiwango kikubwa cha elimu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo