Wananchi watakiwa kulinda miundombinu


Is-Haka Omar, Zanzibar

Zanzibar
NAIBU  Katibu  Mkuu   wa  CCM Zanzibar,  Dk Abdulla Juma  Saadalla ‘Mabodi’, amewasihi  wananchi  wa  shehia ya Ndagoni  mkoani Kusini Pemba kulinda miundombinu ya majisafi na salama isiharibiwe na baadhi ya watu wenye tabia  ya kuhujumu  miundombimu hiyo kwa makusudi.

Nasaha hizo  alizitoa jana wakati  akikagua  miundombinu ya maji iliyotengenezwa na Mamlaka ya Maji Pemba baada ya kuharibiwa na watu wasiojulikana  ambayo  kwa sasa  imerudiswa hali ya kawaida na wananchi  wameanza kupata  huduma hiyo.

Dk Mabodi  alisema nishati ya maji ni muhimu kwa maisha ya kila siku kwa wananchi wote, hivyo ni lazima miundombinu yake ithaminiwe na kuwekewa ulinzi wa kudumu  kwani  ikikosekana  wanaoteseka ni wananchi wasio na hatia hasa wagonjwa na wazee wasiojiweza.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwambia wananchi hao kuwa siasa za chuki na migogoro zimepitwa na wakati, hivyo  wabadilike  na kuanza kuishi kwa misingi ya umoja  na ushirikiano kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya  kisiwa hicho.

Aidha, alieleza kwamba dhamira ya CCM ni kufanya siasa zenye ushindani wa kutatua kero za wananchi, ili kupata huduma bora za kijamii zitakazonufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha,  Dk Mabodi   alitoa  pole kwa wananchi wa kisiwa cha Pemba waliopata mafuriko ya mvua kubwa za masika na kusababisha uharibifu wa mali na vifo, na kwamba  CCM inashirikiana na Serikali kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hao.

“Mwezi uliopita nilikuja hapa na kutoa agizo kwa ZAWA washughulikie tatizo hili na wananchi wapate maji safi na salama, nakupongezeni kwa kutekeleza agizo langu kwa wakati na naendelea kupita maeneo  mengine kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema Dk Mabodi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo