Wanawake CCM wahimizwa kugombea


Is-Haka Omar, Zanzibar

UMOJA wa Wanawake wa Tanzania (UWT) umewataka wanawake kuchangamkia fursa za uongozi kwnye uchaguzi unaondelea sasa ndani ya CCM na jumuiya zake.

Mwito huo ulitolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo Zanzibar, Tunu Juma Kondo katika mwendelezo wa ziara ya UWT kuzungumza na viongozi wapya wa ngazi za matawi kwenye jimbo la Kijini, wilaya ya Kaskazini A, Unguja.

Aliwaambia wanawake kuwa uchaguzi unaoendelea kwenye taasisi hiyo ndiyo fursa mojawapo ya wanawake kupata uongozi ili kufikia malengo ya uwakilishi wa viongozi wenye idadi sawa na wanaume ndani ya chama hicho.

Alifafanua kuwa wanawake wanatakiwa kuondokana na dhana ya kuendelea kuongozwa katika kila nafasi ndani ya CCM bali wajiongeze kuwania uongozi ili kuleta maendeleo endelevu ndani ya chama na jumuiya zake.

Pia alisisitiza viongozi hao kuwa, pamoja na majukumu ya kiuongozi waliyonayo ni lazima wahamasishe kwa wingi wanawake kuwania uongozi ili kupata viongozi makini na wenye uwezo wa kwenda na kasi za kiutendaji za chama hicho.

"Wanawake wenzangu tutumie fursa ya uchaguzi wa chama kuwania uongozi, tusisubiri uteuzi tusimame kupambana na kuhakikisha nasi tunakuwa na nyadhifa kama walivyo wanaume, kwani tunaweza bila kuwezeshwa,’’ alisema Tunu.

Akizungumza kwenye ziara hiyo, Katibu Msaidizi wa Idara ya Organaizesheni ya UWT Zanzibar, Mgeni Ottow alisema CCM itadumu madarakani endapo viongozi wanaopatikana kupitia uchaguzi wa chama hicho watakuwa na uzalendo wa kweli katika kulinda maslahi ya taasisi

Mgeni aliwasihi wanawake wa Umoja huo kuhakikisha wanachagua viongozi waadilifu na wenye uwezo wa kubuni fursa za maendeleo zitakazonufaisha wanawake wenzao na chama kwa ujumla.

“Wanawake ndilo tegemeo la chama chetu na jumuiya kwa ujumla hivyo lazima tuwe wa kwanza kujitokeza kwa kila tukio kuhusu uimarishaji wa chama chetu hasa michakato ya uchaguzi na tukiwa wengi katika nafasi za uongozi, ndipo tutakapopata nguvu za pamoja kutetea haki zetu na kupinga kisheria udhalilishaji wanawake,” alisema Mgeni.

Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Miza Ali Kombo alisema uchaguzi wa ngazi ya wodi unaendelea vizuri, kwani wagombea tayari wamejaza fomu na kinachosubiriwa sasa ni upigaji wa kura ili kupata viongozi watakaoongoza ngazi hiyo kwa miaka mitano.

Katibu wa UWT wa Tawi la Muange, Waja Mnadhani Ali alisema maratajio yake baada ya kupata nafasi hiyo, ni kufanya kazi za jumuiya na chama kwa umakini na uadilifu, ili kuwawakilisha vema wanawake waliomwamini na kumpa ridhaa.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo