Kafulila ataja vikwazo vya mikopo


Celina Mathew

David Kafulila
MBUNGE wa zamani wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ametaja vikwazo viwili vinavyosababisha nchi kukosa mikopo wa wahisani ya kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo iliyopangwa tangu mwaka jana hadi sasa.

Vikwazo hivyo ni mgogoro wa Zanzibar, ukandamizaji wa demokrasia na vikwazo kwa wafanyabaishara huku akiishauri Serikali kuhakikisha inamaliza changamoto hizo na kupata mikopo ya bei nafuu.

Akizungumza jana baada ya taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu mwenendo wa Uchumi na Bajeti Tanzania iliyotolewa hivi karibuni Kafulila alisema Bajeti ya Mwaka 2017/18 haitatekelezeka kama nchi itaendelea kukosa mikopo ya nje.

Alisema Serikali inapaswa kushughulikia mgogoro wa Zanzibar na kusitisha ukandamizaji wa demokrasia ili iendelee kupata mikopo nafuu kwani ni moja ya vigezo vya kupata mikopo hiyo.

Alisema Tanzania inaweza kupata mikopo nafuu ya hadi dola bilioni 2.5 sawa Sh trilioni 6 kwa mwaka, ambapo ni kiasi cha kutosha kwa Serikali kumudu miradi ya kimkakati kama ujenzi wa reli, umeme na bandari.

Pia, lazima Serikali ikae na wafanyabiashara na kuwahakikishia kwamba Tanzania ni sehemu salama kuwekeza na hivyo waweze kuingiza mtaji zaidi, kwani uchumi wa viwanda hauwezi kujengwa kama haipatikani mitaji kutoka kwenye Uwekezaji wa Moja kwa Moja wa Nje (FDI ).

Kafulila alisema kwa muda sasa kwa nchi imekuwa vigumu kupata mikopo nafuu kutokana na masharti yake ya demokrasia na utawala bora.

Alisema mikopo ya kibiashara kutoka nje imeendelea kuwa migumu kutokana na taasisi za kimataifa kuanza kuisoma Serikali kuwa si rafiki wa mazingira ya biashara.

Aliongeza kuwa mbaya zaidi hatujafanya riba za mikopo ili kuhakikishia wawekezaji na benki kwa maana ya kupata mikopo kama ilivyokwishafanyika Kenya na Rwanda kwa upande wa Afrika Mashariki.

“Mazingira yalivyo ni vigumu kupata mkopo kuendesha bajeti na ndiyo maana Serikali imezidi kukopa ndani na kufanya deni la ndani kwenda juu na kuvunja rekodi tangu awamu ya tatu,” alisema.

Alisema awamu ya tatu iliacha deni la ndani la Sh trilioni 1.7, miaka 10 ya awamu ya nne deni la ndani lilifikia Sh trilioni 7.5 mwaka juzi, sasa miaka miwili tu, deni limefika zaidi ya Sh trilioni sawa na nyongeza ya Sh trilioni 3.5 kwa miaka miwili.

“Hii ni hatari sana kwenye nchi ambayo mzunguko wa fedha ndani uko chini mno. Hali ikibaki ilivyo, nchi itazidi kuzama kiuchumi kwa kushindwa kugharimia mahitaji ya afya, maji na elimu kwa sababu ukiangalia deni lililoiva mwaka jana ilikuwa Sh trilioni 8 wakati mwaka huu ni Sh trilioni 9.

Alisema wakati deni hilo likiongezeka hadi Sh trilioni 9 bado mshahara ni Sh trilioni 7.6 na kwamba hiyo inamaanisha kuwa jumla inakuwa ni Sh trilioni 16.6.

Alisema katika mazingira ya sasa ambayo kodi inayokusanywa kwa mwezi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni wastani wa Sh trilioni 1.1 hadi Sh trilioni 1.2, si zaidi ya Sh trilioni 14 kwa mwaka.

Alisema hiyo inamaanisha kwamba makusanyo ya kodi hayatoshi kumudu deni la mshahara kwakuwa tunakopa kwa ajili ya kulipa mishahara wakati gharama za kuendesha serikali na miradi ya maendeleo haijazungumziwa.

Alitolea mfano China ambayo ni Taifa la pili kwa ukubwa wa uchumi duniani baada ya Marekani ambazo pamoja na msimamo wake wa Ujamaa, imefikia ilipo kwa kuwa nchi ya pili baada ya kuwekeza zaidi kwenye elimu, ufundi na teknolojia.

Alisema mtaji mkubwa uliojenga uchumi wa China ulitoka nje hususan Marekani na kwamba lazima ujengwe uchumi wa kisasa kwa kuangalia maendeleo ya dunia na kurekebisha mazingira ya kibiashara.

Alisema mazingira hayo yakirekebishwa na kujengwa imani kwa wawekezaji, mitaji na mikopo itapatikana zaidi ili kuelekea ndoto ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2025.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Poverty and Human Development ya mwaka 2014 ili tufikie dira hiyo, lazima pamoja na mambo mengine tuajiri walimu 900,000 sawa na wastani wa walimu 90,000 kila mwaka.

“Leo ajira za walimu tumeajiri sana mwaka juzi hawakuzidi 30,000, kilimo kinachoajiri asilimia 70 sasa kinakua kwa asilimia 1.7, kiasi ambacho nchini kupata kutokea tangu Uhuru,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo