Warioba: Madini yasitugawe

*Ataka viongozi wasilaumiane kwa yaliyotokea

Mwandishi Wetu

Jaji Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ameonya malumbano na kulaumiana yanayoendelea baina ya viongozi kuhusu madini na rasilimali nyingine za taifa akisema yanaweza kuligawa Taifa.

Aidha, Warioba ambaye alikuwa pia Makamu wa Kwanza wa Rais amesema yupo tayari iwapo Rais John Magufuli atamhitaji kwa ajili ya ushauri wenye lengo la kurutubisha sera, sheria na utendaji katika rasilimali za Taifa kwa faida ya Watanzania wote.

Akizungumza katika mahojiano kwenye ofisi zake zilizopo Osterbay Dar-es-Salaam kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi na rasilimali za Taifa, Jaji Warioba alisema ni muhimu sasa viongozi wakaacha kulaumiana na badala yake waweke kando tofauti zao kwa ajilin ya kutafuta namna ya kujenga Taifa.

Warioba alisema hayo alipokuwa akijibu swali lililotaka kujua maoni na mapendekezo yake kwa viongozi wote kuhusu madini pamoja na Rais John Magufuli kwa hatua zake katika sekta hiyo.

“Naliona hili la malumbano yatatugawa, (viongozi) waache tofauti zao. Hii lawama ya madini ingekuwa ni mwanzo kwa kuleta mawazo na maoni ya kutengeneza katika kulinda na kuzitumia rasilimali zote kwa maendeleo ya Taifa letu,” alisema Warioba na kuongeza:

Jambo la msingi ni kutafuta suluhu itakayotupeleka mbele, tuone sera zetu zikoje na zinatusaidiaje kulinda rasilimali za Taifa, tunarekebisha vipi kuondoa tatizo, sheria na utendaji kwa ujumla. Naomba Watanzania tutoe maoni na mawazo yatakayoboresha sera, sheria na utendaji au usimamizi wa rasilimali husika. Tunaweza kurudisha miiko na maadili ya uongozi katika kusimamia rasilimali za nchi, kila Mtanzania ajue sio mali yake ni ya Watanzania wote, lazima aitunze vinginevyo atahukumiwa kwa hilo.”

Alisisitiza: “Viongozi msaidieni Rais kulishughulikia kwa pamoja. Hili si jambo la chama wala taasisi. Hakuna haja ya kupeana lawama, ukishasema tumekosea unatakiwa ueleze tufanye nini, sio kusema Serikali ichukue hatua, kwani Serikali ni nani, si mimi na wewe. Sasa kwa nini wewe hutaki kulitolea maoni?”

Akionya na kusisitiza haja kwa viongozi kuacha malumbano na kulaumiana Warioba alisema: “Tujiamini, nimeona katika malumbano hayo, wengine wanaonekana kama hatujiamini kama tukifanya hivi tunaweza kushitakiwa, mabadiliko yoyote yana machungu yake. Tusije tukapoteza imani tuliyonayo, tunaweza tukapoteza mapato yetu, lakini ni lazima tufanye kwa kujenga afya ya rasilimali zetu.”

Alisema kutokana na hatua ya Rais kukutana na mmiliki wa Barick ingawa kila upande una msimamo wake ni vyema kuiachia suala hilo Serikali na kwamba ni Imani yeke itafanikiwa.

Hata hivyo alisema anashangazwa na mazungumzo ya baadhi ya viongozi wanaotaka Serikali ihakikishe inazipata takriban Sh trilioni 108 zilizotajwa kwenye taarifa ya kamati ya Profesa Osoro akisema mawazo hayo si sahihi.

“Nadhani hili si sahihi, tuna imani na viongozi wetu wakuu hasa Rais, lolote litakaloafikiwa tulipokee na kulikubali tusije kuanza kulumbana ripoti imesema trilioni 108 ziko wapi? Pia nilisemee hili la dalili za kupoteza imani, eti tukifanya hivyo tutashitakiwa sababu ya mikataba na wawekezaji hawatakuja. Mimi naamini watakuja tu, rasilimali zipo kwetu hawana jinsi,” alisema Warioba.

Msaada wake kwa Rais

Alipotakiwa kueleza ana msaada gani kwa Rais Magufuli, Warioba aliyeongoza Tume ta Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba Mpya alisema: Sisi tupo, Uongozi ni suala la kupeana vijiti, unafika mahali unangatuka watu wanadhani kungatuka ni kustaafu hapana si sahihi:

Wazee hawaingii katika mambo ya vijana, sisi tupo lakini hatutaki kuingilia utendaji wao kama sisi tulivyoachiwa kuendesha nchi, ila Rais akituhitaji tupo tayari kwa ajili ya ushauri anaweza kuukubali au kuukataa. Nataka nimhakikishie kwa hili tupo pamoja na tutatoa maoni ya kurutubisha sera, sheria na utendaji katika rasilimali za nchi hii.”

Akizungumzia kauli ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kutaka madini yaachwe mpaka Watanzania watakapokuwa na ufahamu wa kutosha ndipo wataamua kuyachimba, Warioba alisema kiongozi huyo alitoa kauli hiyo baada ya uhuru akiwa hana wataalamu zaidi ya madaktari wawili na yeye mwenyewe hivyo alikuwa sahihi kwani angeruhusu hilo Watanganyika wangekuwa watazamaji tu bila kufaidika na lolote.

Akijibu swali lililotaka kujua nini tatizo kwa Tanzania kuhusu rasilimali na hatua za kuchukua, mwanasiasa na mbobezi huyo wa sheria alisema haoni kama kuna tatizo la msingi bali ni uelewa na imani ya watu kwa viongozi.

“Sioni kama kuna tatizo la msingi lakini, ni suala la uelewa mara nyingi kuna watu ambao huamini viongozi wao kwa kila kitu wanachosema. Lazima wananchi wawe makini kwa sababu tatizo la Watanzania ni maendeleo kila mwananchi ana kiu ya kutaka tufikie mahala pazuri kama Taifa na mimi nakubaliana nao kabisa. Tuna rasilimali nyingi, ambazo kimsingi tukiweza kuzishughulikia kwa makini kama lilivyoshughulikiwa suala la mchanga wa madini tutakuwa mbali sana kiuchumi,” alisema.

Akishauri alisema: “Tuangalie rasilimali ya madini kwa mapana yake na kushughulikia wawekezaji wa ndani na wale wa nje, Barick na Acaccia ni sehemu ndogo sana ya madini, tuangalie wachimbaji wa ndani, mfano; Tanzanite ni aibu, madini yanachibwa Manyara biashara hii inatokaje Mererani na kufanyika Nairobi na New Delhi. Tujiulize kwa nini sio Arusha na Dar-es-Salam?”

Alishauri pia kuangaliwa na kujadiliwa kwa Taifa linavyoweza kunufaika zaidi na rasilimali zitokanazo na bahari, maziwa na mito pamoja maliasili za wanayamapori, mbuga za wanyama, vitalu vya utalii na ardhi.

“Unampaje mfanyabiashara kibali cha kuwinda miaka 99 yaani atumie yeye, wanawe na wajukuu zake, Watanzania watatumia lini, haya ni masuala ya msingi kabisa ya kuangalia upya. Lakini tusijidanganye bishara ya madini hata mafuta ina changamoto kubwa duniani hususan Afrika, biashara hii unapambana na watu wenye fedha popote utakapokwenda, uchumi unategemea mafuta na madini utaona jinsi wakubwa wanavyooneemeka na rasilimali hizo na kuwaaacha wananchi wakiwa masikini, mfano mzuri Nigeria,”alisema Warioba.

Pamoja na kuangalia maadili na nidhamu lazima kuwe na uwazi katika mikataba ni muhimu sana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo