Wahariri washtushwa na Serikali kufunga Mawio


Suleiman Msuya

Viongozi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kushtushwa, kuhuzunishwa na kushangazwa kwake na hatua ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe kulifungia kwa miaka miwili gazeti la kila wiki la Mawio, adhabu iliyoanza Juni 15, 2017.

Aidha, TEF imesema itaendelea kupinga vitendo vya uonevu dhidi ya vyombo vya habari ambavyo siyo tu kwamba vinakandamiza uhuru wa habari, bali vinavunja Sheria inayosimamia sekta ya habari nchini.

Akitoa tamko la chombo hicho kuhusu uamuzi wa Waziri Mwakyembe kufungia gazeti hilo jana, Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga alisema kitendo cha Serikali kufungia Mawio si sahihi na kwamba hata sababu zilizoanishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dk. Hassan Abbasi hazikuwa na tija kwa maslahi ya Taifa.

Makunga alisema kufungia gazeti kutokana na kuchapisha katika ukurasa wake wa kwanza na ule wa 12 picha na habari zinazowahusisha marais wastaafu; Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete na usafirishaji wa mchanga wa dhahabu nje ya nchi bila kuanisha ni kifungu gani cha sheria kimevunjwa si sahihi.

Mwenyekiti huyo alisema TEF baada ya kupitia taarifa ya Serikali ya Juni 15, 2017 iliyotangaza kulifungia Gazeti la Mawio kwa miaka miwili (2), limebaini Waziri Mwakyembe amekiuka Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 kwa kujivika mamlaka ya Kimahakama ambayo kimsingi hana kwa mujibu wa sheria hiyo.

“Vifungu vya sheria vilivyotajwa katika tarifa ya serikali havimpi waziri mamlaka wala wajibu wakufungia chombo chochote cha habari,” alisema.

Alisema kifungu cha 59 cha Sheria hiyo kinatoa mamlaka kwa waziri kuzuia maudhui katika habari na siyo kufungia chombo cha habari kama waziri alivyofanya.

Makunga alisema maudhui yanayopaswa kuzuiwa na waziri kwa mujibu wa kifungu hicho ni yale yanayohatarisha usalama wa nchi au usalama wa umma.

Alisema tuhuma kwamba Mawio lilikiuka vifungu namba 50 (a), (b), (c), (d) na (e) vya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 si za kweli, kwani sehemu hiyo ya sheria inataja makosa ambayo mwandishi wa habari anaweza kutiwa nayo hatiani ikiwa atafikishwa mbele ya Mahakama.

“Vifungu hivyo vinahitimishwa kwa adhabu inayotolewa na sheria kwa makosa husika. Adhabu hizo ni faini kati ya Sh.milioni 5 na Sh. milioni 20 au kifungo jela kati ya miaka mitatu na miaka mitano au vyote kwa pamoja,” alisema.

Alisema makosa yanayotajwa yanaweza kuthibitishwa tu ikiwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa kuwa waziri siyo mahakama, hana mamlaka ya kisheria ya kuwatia hatiani Mawio na hawezi kuwa rejea ya makosa yaliyotajwa katika sheria hiyo.

Aidha, alisema habari katika ukurasa wa 12 wa gazeti la Mawio ambayo inadaiwa kuwa ilichapishwa kinyume cha maagizo na maelekezo ya serikali, ilinukuu kauli ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ndani ya Bunge.

Mwenyekiti huyo wa TEF alisema waziri anapaswa kukumbuka kuwa mijadala ya Bunge na kauli za wabunge ndani ya Bunge ni miongoni mwa mambo yanayotajwa katika Kifungu cha 38 cha Sheria ya Habari ya 2016 kwamba yanaweza kunukuliwa kama yalivyo bila kujali ukweli au uongo wake.

“Kwa maana hiyo, hatua ya kulifungia Mawio kwa kuandika taarifa zilizotokana na Bunge, pia ni kukiuka sheria inayosimamia sekta ya habari,” alisema.

Alisema ni dhahiri kwamba mchakato mzima wa kulifungia gazeti la Mawio umekiuka Sheria ya Huduma za Habari ya 2016 ambayo Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa inalenga kusimamia weledi katika sekta ya habari.

Alisema TEF inahuzunishwa na utamaduni uliojengeka miongoni mwa viongozi na watendaji wakuu wa wizara ya habari kwamba adhabu pekee ya kukimbilia ni kufungia vyombo vya habari.

Alisema uamuzi huo unaondoa dhana nzima ya malezi na mashauriano na mwenendo huo hauna afya kwa sekta ya habari na nchi yetu.

Makunga alisema TEF inatoa wito kwa gazeti la Mawio kutafuta haki yake kama walivyowahi kufanya wakati gazeti hilo lilipofutwa Januari 2016 na baadaye kurejeshwa na Mahakama.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo