Wapelelezi wahimizwa kuepuka rushwa


Mwandishi Wetu

Mama Samia Suluhu Hassan
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wapelelezi na waendesha mashitaka nchini kuepuka rushwa na wafanye kazi kwa bidii kwa kutanguliza maslahi ya nchi kwa kuchukua hatua stahiki dhidi ya wezi wa rasilimali za Taifa.

Samia alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati akizindua mwongozo kwa wapelelezi na waendesha mashitaka wa kesi za wanyamapori.

Taarifa zinaonesha kuwa watuhumiwa 13 wa makosa ya ujangili wa thamani ya Sh milioni 800 wengi wakiwa wageni waliofikishwa katika mahakama za Dar es Salaam walitoroka.

Alisema mwongozo aliozindua utasaidia uboreshaji upelelezi na uendeshaji kesi kuhusu wanyamapori na misitu nchini.

“Uwepo wa mwongozo huu ni dhahiri utatoa matokeo chanya katika mapambano dhidi ya ujangili na uhalifu wa misitu yetu,” alisema Samia.

Alisema ana imani mwongozo huo utakomesha uhalifu ambao umekuwa ukiisababishia Serikali hasara kubwa ikiwamo ya uharibifu wa rasilimali za Taifa na kupoteza mapato ambayo yangesaidia kuimarisha huduma za kijamii nchini.

Kuhusu sekta ya utalii, Makamu wa Rais alisema pamoja na sekta hiyo kuliingizia Taifa mapato mazuri, inasikitisha kuona wanyamapori wanazidi kupungua hivyo kuwa tishio kwa uchumi na nchi.

Alisema ujangili umeendelea kuangamiza wanyama hasa tembo, hivyo ni muhimu kwa wapelelezi na waendesha mashitaka kutenda haki bila kuonea mtu kwa wanaokamatwa wakifanya vitendo hivyo ili viweze kukomeshwa nchini.

“Wazee wetu walilinda na kutunza rasilimali zetu kwa faida yetu, nasi tuzitunze kwa ajili ya vizazi vijavyo,” alisema Samia.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alimhakikishia Makamu wa Rais kuwa mapambano dhidi ya ujangili na utoroshaji wanyama na viumbe wengine yatakuwa endelevu na watakaokamatwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Profesa Maghembe alimwomba Mkuu wa Jeshi la Polisi, Simon Sirro kuendesha oparesheni maalumu ya kukusanya silaha zinazotumika kwa ujangili ili wanyama hasa tembo wawe salama kwenye maeneo ya hifadhi za Taifa nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwendesha Mashitaka, Mkuu wa Serikali, Biswalo Mganga alisema katika kipindi cha mwaka 2014/17 ofisi yake ilifikisha mahakamani washitakiwa wakubwa wa ujangili ambao wamekuhumiwa vifungo virefu na faini.

Alisema washitakiwa 100 walihukumiwa kulipa faini ya zaidi ya Sh bilioni 1.1 kwa kujihusisha na nyara za Serikali kinyume na sheria na faini hizo zililipwa serikalini.

Alisema katika idadi hiyo, watuhumiwa zaidi ya 80 walihukumiwa kifungo cha miaka 20 hadi 30 gerezani na faini ya zaidi ya Sh milioni 164 ambazo bado hazijalipwa serikalini.

Biswalo alisema mafanikio hayo yote yamechangiwa na usimamizi madhubuti wa kesi hizo kupitia dawati la wanyamapori katika Divisheni ya Mashitaka na mawakili wa Serikali katika ofisi zote za mikoani.

Hata hivyo, alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye kazi kwa sasa ni dhamana kwa watuhumiwa wakubwa wa vitendo vya ujangili ambapo utafiti unaonesha kuwa mahakama za Dar es Salaam pekee kati ya mwaka 2010 na mwaka juzi 2015 kulikuwa na mashauri 13 yanayohusu nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 800.

Nyara hizo zilikamatwa ndani na nje ya nchi ambapo watuhumiwa   walipewa dhamana na kutoweka.

Biswalo alisema katika mashauri hayo, asilimia 69 ni raia wa kigeni na asilimia 31 ni wa Tanzania.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo