Serikali: Mabaki ya Dinosaria kurudishwa si tija


Octavian Kimario, Dodoma

Ramo Makani
SEIKALI imesema wazo la kuwarudisha nchini Dinosaria kutoka Ujerumani halina tija kutokana na ugumu wa kiteknolojia na gharama ikilinganishwa na faida za hatua hiyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani akijibu swali la Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu faida ambayo wananchi wa Lindi na Tanzania kwa jumla wanaipata kutokana na mabaki hayo.

Makani alisema Tanzania itaendelea kusisitiza kupata manufaa kutokana na Dinosaria wake walioko Berlin, Ujerumani.

“Kutokana na majadiliano ya kina yaliyohusisha wataalamu wabobezi katika masuala ya malikale kutoka pande zote mbili, ilikubalika kuwa Serikali ya Ujerumani itaendesha shughuli za utafiti zaidi Tendaguru na maeneo jirani.

“Nia ni kuwezesha uchimbaji mabaki ya Dinosaria wengine yanayoaminika kuwepo maeneo hayo pamoja na kuanzisha Kituo cha Makumbusho ili shughuli za utalii zifanyike eneo hilo na kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi,” alisisitiza Makani.

Kuhusu Serikali kupunjwa mapato yatokanayo na viingilio kwenye Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin, Makani alisema jambo hilo halina ukweli.

Alisema ni ngumu kufahamu kiasi ambacho hupatikana kutokana na kiingilio kuwaona mijusi wa Tanzania, kwa kuwa Makumbusho hayo yana kumbi nyingi zenye masalia kutoka nchi kadhaa za Afrika na gharama za kuendesha Makumbusho hayo hutolewa na Serikali ya Ujerumani.

Alieleza kuwa Serikali hiyo itafadhili uimarishaji wa idara inayohusika na malikale katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwezesha upatikanaji wataalamu wa kutosha wa fani hiyo ili kuendeleza utalii wa malikale nchini.

Mabaki ya mijusi hayo wakubwa (Dinosaria) yalichimbwa kwenye kilima cha Tendaguru mkoani Lindi kati ya mwaka 1909 na 1913 na kupelekwa kwenye Makumbusho ya Elimu Viumbe ya Berlin.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo